Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton hapo Alhamisi
(tarehe 17 Januari) alitangaza rasmi kutambuliwa kwa serikali ya Somalia
na Marekani baada ya mkutano na Rais Hassan Sheikh Mohamud mjini
Washington.
"Watu na viongozi wa Somalia wamepigana na kujitoa muhanga kwa ajili
ya kuleta utulivu, usalama na amani kwa taifa lao," alisema Clinton.
"Bado kuna safari refu ya kwenda na changamoto nyingi za kuzikabili,
lakini tumeona ukiwekwa msingi mpya wa kujengea mustakabali mwema."
Marekani haijawahi kuitambua serikali ya Somalia tangu mwaka 1991, na
Clinton alisema kwamba nchi yake sasa inatazamia "mdahalo wa wazi juu
ya kile tunachoweza kufanya kuasaidia watu wa Somalia kutimiza ndoto
zao."
"Kwa mara ya kwanza ndani ya miongo miwili, nchi hii ina serikali
inayowawakilisha wananchi na rais mpya, bunge jipya, waziri mkuu mpya na
katiba mpya," alisema.
Mohamud alizungumzia matumaini yake kwa mustakabali wa Somalia.
"Tunapigania kuwa na Somalia ambayo ina amani ndani yake na majirani
zake, ambayo raia wake wanaweza kufanya shughuli za kila siku kwa
usalama," alisema. "Ukosefu wa utulivu, siasa kali za vurugu na uhalifu
nchini Somalia ni kitisho sio tu kwa Somalia bali pia kwa eneo zima na
ulimwengu kwa ujumla. Tunauangalia mustakabali wetu kwa matumaini,
fahari na matarajio."
"Somalia inashukuru sana kwa msaada mkubwa wa Marekani kwa watu wa
Somalia," alimwambia Clinton, baada ya mkutano wake wa awali na Rais
Barack Obama.
No comments:
Post a Comment