Watu wenye silaha ambao hawakutambuliwa walimuua mtangazaji wa radio
wa shirika la Shabelle Media Network (SMN) mjini Mogadishu hapo Ijumaa
(tarehe 18 Januari), liliripoti shirika la habari la AFP.
Abdihared Osman Adan alipigwa risasi mara kadhaa alipokuwa akielekea
kazini kutoka nyumbani kwake katika wilaya ya Wadajir ya Mogadishu.
"Watu wenye silaha walimpiga risasi mara tatu shingoni na begani.
Alijeruhiwa vibaya na alipelekwa hospitali ambako alitangazwa
ameshafariki dunia," alisema mfanyakazi mwenzake Mohamed Bashir.
"Hatujui dhamira ya wauaji hao, lakini inaonekana kuwa ni sehemu ya
kampeni ya kuumaliza uhuru wa habari nchini."
Abdihared Osman Adan ni mwandishi wa habari wa kwanza wa Kisomali kuuawa katika mwaka huu wa 2013. Waandishi 18 wa habari waliuawa nchini Somalia mwaka jana,
wakiwemo wanne wanaofanya kazi na shirika la SMN, miongoni mwao akiwa
ni mkurugenzi wa stesheni hiyo. Hakuna mtu hata mmoja aliyefikishwa
mahakamani kwa mauaji hayo.
Shirika la SMN liliyalaani mashambulizi hayo likisema kwamba Adan
alikuwa "mfanyakazi wa kipekee na anayeshughulika kote kwenye
televisheni na redio wa mtandao huo."
Balozi wa Uingereza nchini Somalia Matt Baugh kwa haraka aliitaka
serikali ya Somallia kuwafikisha wauaji mbele ya sheria. "Ni muhimu
kumaliza hii hali ya watu kutokuguswa na mkono wa sheria kwa mauaji ya
waandishi wa habari," alisema, kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwenye
mtandao wa Twitter. "Kazi yao ni muhimu sana kwa mustakabali wa Somalia
na lazima waweze kufanya kazi bila ya kuhofia maisha yao. Ninawapongeza
kwa ushujaa na taaluma yao."
No comments:
Post a Comment