Thursday, January 17, 2013

Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia kuchunguza vifo vya raia Lego

Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) ilisema inachunguza mauaji ya hivi karibuni ya raia waliojikuta katikati ya mapigano baada ya wanamgambo wa al-Shabaab kuvishambulia vikosi vya AMISOM karibu na eneo la Lego lililoko umbali wa kilomita 129 magharibi ya Mogadishu.
Ripoti za awali zinaonesha kwamba watu wazima na watoto waliuawa na kujeruhiwa katika tukio hilo la hapo Jumanne (tarehe 15 Januari), ilisema taarifa ya AMISOM.
"AMISOM iko makini na jukumu lake la kupunguza madhara dhidi ya raia wakati wa operesheni zake na tuna kanuni za wazi kabisa za kukabiliana na wapiganaji kwenye hali kama hiyo," alisema Kaimu Kamanda wa Kikosi hicho, Meja Jenerali Salvatore Harushimana. "Kwa hivyo kwa sasa tunachunguza ukweli na hali iliyozunguka tukio hili la kuhuzunisha ili kufahamu ikiwa na kwa kiasi gani kanuni hizo zilivunjwa."
Tukio kama hilo lilitokea mwezi Oktoba, pale kiasi cha raia sita walipouawa basi lao lilipopita kwenye eneo la mapigano kati ya al-Shabaab na AMISOM huko Lego.

No comments:

Post a Comment