Thursday, January 17, 2013

Watu wasiopungua 4 wafa katika mashambulizi kwenye mkahawa Garissa

Watu wasiopungua wanne waliuawa, akiwemo afisa wa ngazi za juu wa polisi, na sita kujeruhiwa vibaya pale watu wenye silaha walipoushambulia mkahawa mmoja mjini Garissa siku ya Jumatano (tarehe 16 Januari).
"Watu wanne walikufa hapo hapo, ambapo wengine sita walipelekwa kwa haraka hospitali," Mkuu wa Jimbo la Garissa, Mohamed Maalim, aliliambia shirika la habari la AFP. "Washambuliaji waliuvamia mkahawa ambapo walinzi walikuwa wakila chakula cha jioni na kufyatua risasi ovyo ovyo na kisha kutoroka."
Naibu mkuu wa gereza la Garissa, Allan Njagi, alikuwa miongoni mwa waliokufa, liliripoti gazeti la The Standard la Kenya.
Polisi wanawashuku wafuasi wa al-Shabaab walioko Garissa kufanya mashambulizi hayo na mengine ya hivi karibuni, ingawa kundi hilo la wanamgambo bado halijadai kuhusika. Hata hivyo, kundi hilo limetoa kiwango kikubwa cha bahashishi kwa kuuliwa maafisa usalama wa Kenya katika jaribio la kuwaandikisha vijana wengi zaidi wa Kenya.
Hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, alisema mkuu mpya wa polisi wa eneo hilo Charlton Mureithi.
Washukiwa wawili wa kujitoa muhanga pia waliuawa siku ya Alhamisi asubuhi karibu na kambi ya Hagadera kwenye kambi za wakimbizi za Dadaab pale mabomu yao yalipolipuka zikiwa mikononi mwao, alisema.
Mureithi alisema anashuku kwamba mabomu hayo yalikuwa yategwe barabarani ili kuvilenga vikosi vya usalama.
Mji wa Garissa na vitongoji vyake umekuwa ukikabiliwa na matukio kadhaa ya ghasia ikiwemo mashambulizi ya maguruneti na ufyatulianaji wa risasi katika miezi ya hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment