Jan
31
2013
MBUNGE mstaafu wa Kwela,Sumbawanga mkoani Ruvuma, Chrisant Mzindakaya ameitaka katiba ilinde Muungano, kwa madai kuwa ukivunjika madhara yake kwa usalama wa nchi ni makubwa kuliko bomu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kuwasilisha maoni yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mzindakaya alisema kuwa hasara ya kuvunjika kwa Muungano ni kubwa kwani ni uhai wa taifa.
“Muungano ukivunjika tutatafutana hapa, kutakuwa na ugomvi na hasara itakayopatikana ni kubwa na nchi za Magharibi watafurahi maana watatugawa na hapo uvamizi wa rasilimali utazuka,” alisema.
Mzindakaya ambaye ameshika wadhifa wa ubunge kwa miaka 40, alisema kuwa amependekeza katiba mpya iandaliwe kwa maslahi ya nchi na kuitaka tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, kutokubali maoni ya viongozi wanaotamani vyeo.
Alisema katiba hiyo iifanye nchi izaliwe upya ikiwemo rasilimali za nchi kuwa za Watanzania na mmiliki awe serikali.
“Ardhi, madini, gesi na maliasili zote zinaweza kuwekezwa, lakini wananchi wakamiliki asilimia 46, na lazima katiba ilinde wazalendo ili watu wasiwe watumwa katika nchi yao.
“Nimependekeza katiba ikatae biashara ya chumvi, maua eti mwekezaji katoka nje ya nchi, sasa sisi tufanye kazi gani? Nimetaka wawekezaji wasajiliwe,” alisema.
Alisema kuwa amependekeza rais asipewe nafasi ya kuchagua wabunge kumi wakiwemo wa viti maalumu, badala yake wapigiwe kura na si kuchaguana kama wafanyavyo sasa.
Naye Mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya, amependekeza katiba mpya itamke wazi rasilimali za nchi ni mali ya wananchi na itamke mrabaha utakaotolewa kwa eneo husika lenye rasilimali hiyo, ili kuondoa migogoro kama ya gesi ya Mtwara na mafuta ya Pemba.
Ngawaiya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (Cegodeta), alipendekeza kuondolewa kwa viti maalumu kwa sababu vinadumaza wanawake na kuchochea rushwa ya ngono ndani ya vyama vya siasa.
No comments:
Post a Comment