Jan
1
2013
MTU mmoja aliyejitambulisha kuwa ofisa usalama wa taifa, juzi usiku alizua balaa katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI), baada ya kutaka kuingia kwa nguvu wodini alikolazwa padri wa kanisa Katoliki, Ambrose Mkenda, aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana hivi karibuni visiwani Zanzibar.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zilisema kuwa ofisa huyo aliyekuwa na bastola, alikuwa akitaka kuingia kwa nguvu wodini humo, lakini walinzi wanaomlinda padri huyo walikabiliana naye vikali wakitaka kujua sababu ya kutaka kuonana naye.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Mkurugenzi wa MOI, Lauwrence Maseru, alikiri kutokea kwa tukio hilo la mtu huyo kufika hospitalini hapo majira ya usiku na kulazimisha kuingia wodini alikolazwa Mkenda.
Chanzo chetu cha habari kilieleza kuwa baada ya kuzuiliwa, ofisa huyo alichomoa bastola kuwatisha walinzi na kulazimisha kuingia.
Maseru alisema kuwa tayari wametoa taarifa polisi ili mtu huyo ashughulikiwe kwani aliingia kinyume cha utaratibu.
“Sasa ulinzi umeimarishwa, kuna askari wawili wawili wanaachiana kumlinda padri tangu lilipotokea jaribio hilo la mtu huyo kutaka kulazimisha kuingia kwa nguvu,” kilisema chanzo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieta Komba, alikanusha akisema kuwa ofisa huyo aliyeingia kwa kulazimisha wodini hakuwa anaenda kumwona Padri Mkenda bali alikuwa anaenda kumwona askari mwingine aliyekuwa wodi moja na padri.
Pia Kamanda Komba alikanusha kuwa hakukuwa na matumizi ya bastola kuwatisha walinzi, akisema kuwa tukio hilo halihusiani na padri.
Chombo kimoja cha habari jana kilimkariri Padri Mkenda akisema kuwa kuna genge la watu ambalo limekuwa likifanya vitendo vya hujuma dhidi ya viongozi wa dini na raia wasiokuwa na hatia Zanzibar.
Padri Mkenda ambaye pia ni paroko wa parokia ya Mpendae, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliyefika hospitalini hapo kumjulia hali.
Desemba 25 mwaka jana, padri huyo alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, hivyo kulazwa kwa muda katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar kisha kuhamishiwa MOI.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment