Dec
31
2012
WATU sita wanaosemekana kuwa majambazi, wamemvamia Mweka Hazina wa Klabu ya Simba, Eric Sekiete (28), Mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam na kumpora sh 7,590,000 pamoja na dola 2,000 za Marekani (zaidi ya sh mil. 3) zilizokuwa ni mapato yaliyopatikana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi yao na Tusker ya Kenya uliopigwa juzi katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP), Charles Kenyela, alisema tukio la kuporwa kwa Sekiete lilitokea majira ya saa 3:30 usiku juzi maeneo ya Sinza Makaburini na baadaye kuripotiwa katika kituo cha polisi Magomeni majira ya saa 5:30 usiku.
Kenyela alisema tukio hilo lilitokea mara baada ya Sekiete na Stanley Philipo (23), mwanafunzi wa Kijitonyama, kushuka katika gari aina ya Corona Premio lenye namba za usajili T 869 BKS lililokuwa likiendeshwa na Said Pamba.
Alisema mara baada ya Pamba kusimama katika eneo hilo, aliwashusha Sekiete na Philipo na mara tu baada ya kuvuka barabara wakitaka kupanda teksi, zilitokea pikipiki tatu zilizokuwa na watu sita, ambapo mmoja wa watu hao wasiofahamika alikuwa na silaha ndogo, ambayo alifyatua risasi juu na kuwapora begi lililokuwa na fedha hizo.
Kamanda Kenyela alibainisha kuwa, mara baada ya waporaji hao kupora begi hilo walisikika wakisema; “Mnafungwa halafu mnatuzingua na kwa kuwa viongozi wenu wanakula pesa za klabu na sisi tunaziiba.”
Aidha, Kamanda Kenyela aliongeza kuwa, fedha hizo zilikuwa ni mali ya Simba, yakiwa ni mapato ya uwanjani yalizosalia mara baada ya kufanyika kwa mgawo wa sh milioni 10.6 na dola 2,000 za Marekani zilizopatikana katika mchezo huo.
Aliongeza kuwa, mpaka sasa Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio hilo, ambao ni Sekiete, Philipo na Pamba kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku wakitaka kujua sababu ya kupeleka mali ya klabu nyumbani bila ya kuihifadhi ofisini. Pia watazungumza na viongozi wa klabu hiyo.
Kenyela alibainisha kuwa, mpaka sasa uchunguzi wa kuwakamata wahalifu hao unaendelea, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwao ili kitendo hicho kiseweze kujitokeza tena, kwani hakifai katika tasnia ya soka hapa nchini.
Katika mchezo huo dhidi ya Tusker ya Kenya, Simba ililala kwa mabao 3-0.
Katika hatua nyingine, mabingwa hao wa soka Tanzania Bara, wanatarajiwa kuondoka nchini Januari 10 kwenda Oman kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
Chanzo cha habari cha uhakika kutoka ndani ya klabu ya Simba, kiliipasha Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina kuwa, maandalizi juu ya safari hiyo yanakwenda sawa, ila wanachosubiri hadi sasa ni ujio wa kocha wao mkuu, Patric Lieweg.
“Mambo yanakwenda sawa, juu ya safari yetu na mpaka sasa tunasubiria tu, siku kufika na wachezaji wetu kwenda Oman kuweka kambi nchini humo, ambapo pia tutacheza mechi za kirafiki si pungufu ya nne ili kuhakikisha kikosi kinarejea vema na kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kutetea ubingwa ambao tunaushikilia hadi sasa, pamoja na michuano ya kimataifa,” alisema mtoa habari huyo.
MTANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment