Jan
30
2013
Imewekwa na Hamed Mazrouy
Watendaji wa jeshi la polisi nchini wameshauriwa kuendeelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ili waweze kuungwa mkono na wananchi katika kulinda amani na utulivu wa nchi.Ushauri huo,umetolewa na Mwakilishi wa jimbo la Uuzini Mh, Mohamed Raza wakati akikabidhi vifaa vya ujenzi na michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa watendaji wa jeshi hilo huko makao makuu ya polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda.
Mh, Raza amesema kuwa jeshi la polisi ni kiungo muhimu cha kudumisha amani katika jamii hivyo wanatakiwa kuzidisha juhudi za kiutendaji katika utekelezaji wa majukumu yao kwa uadilifu.
Aidha amefahamisha kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo ni miongoni mwa kutekeleza ahadi alizozitoa kwa jeshi hilo ili kuhakikisha askari wanafanya kazi katika mazingira mazuri yatakayowasaidia kutoa huduma bora na endelevu kwa jamii.
Nae Kamishna msaidizi wa polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja Ahmada Abdallah Khamis ametoa shukrani zake kwa Mwakilishi huyo juu ya msaada alitoa na kuahidi kuwa utatumika kwa shughuli iliyokusudiwa ili ofisi za jeshi hilo ziwe za kisasa zinazoendana na taswira ya askarin wake.
Pia amesema jeshi hilo limekuwa na ushirikiano mkubwa na wananchi katika kupambana na harakati mbalimbali za uharifu na matukio mengine ya uhalifu ili kuhakikisha zanzibar inazidi kuwa kitovu cha amani duniani.
No comments:
Post a Comment