Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Fowsiyo Yusuf Haji Aadan alianza ziara yake kwa nchi kadhaa wiki hii ili kurekodi mali za Somalia zenye thamani ya kifedha katika mabenki ya nje, pamoja na mali zake za kibiashara, balozi, ndege na meli.
Ya kwanza katika ajenda yake ni safari kwenda Nchi za Falme za Kiarabu, Italia na Uingereza.
"Tutafanya mapitio ya ziada ya mali zote za Somalia duniani katika mabara yote na tutawasiliana na washauri wa kigeni wa fedha na sheria," Aadan aliiambia Sabahi tarehe 27 Disemba. "Serikali ya Somalia itaomba kurejeshewa fedha zilizoshikiliwa na mamlaka za Uswisi pamoja na meli na ndege zilizoko Ujerumani, Italia na Yemeni."
Mamlaka ya Ukaguzi wa Soko la Fedha la Uswisi bado halijaweka wazi upana wa akaunti wa serikali kuu ya zamani ya Somalia au biashara baina ya benki za Uswisi na viongozi maarufu wa Somalia ambao mali zao zilizuiliwa.
Huku kukiwa na machafuko kufuatia kuanguka kwa serikali kuu ya Somalia, baadhi ya serikali za kigeni zilizuwia akaunti rasmi za benki za Somalia ili kuepuka matumizi yasiyoidhinishwa. Hata hivyo, mali nyingi za kuoekana za serikali huko nje, ikiwa ni pamoja na ndege na majengo ya balozi za zamani, tangu wakati huo yamekuwa hayasimamiwi vizuri au haijulikani hesabu zao.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyovuja mwezi wa Julai, usimamizi mbaya wa mali za umma uliendelea wakati wa Serikali ya Mpito ya Shirikisho, ambapo asilimia 70 ya mapato yalipotea kwa ufisadi, wizi au upotevu. Nyingi ya pesa hizi zinashukiwa kuwa zimepelekwa nje.
Waziri wa Fedha Mohamud Hassan Suleiman aliitaka jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi na Somalia kuisadia katika kuzipata tena mali zake zote.
"Hatutasita kuzipata pesa ambazo ziliwekwa visivyo halali katika benki za kigeni, ikiwa ni pamoja na akaunti za benki za serikali zilizopita, na [kuibiwa kutoka] misaada ya kifedha kwa zaidi ya miongo miwili," Suleiman aliiambia Sabahi. "Tutapanga mpango ambao tutawaomba washirika wetu wa Somalia, ikiwa ni pamoja na maafisa wa zamani wa fedha, [kutoa] nyaraka za ufuatiliaji wa fedha hizo."
Mwezi wa Novemba, serikali ilipeleka ombi rasmi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka usaidizi kudai tena fedha na mali nyengine kutoka nchi za kigeni.
Majaribio ya zamani ya kurejesha mali zilizoko nje
Mwezi Disemba 2009, rais wa zamani Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alimteua aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Somalia Ali Abdi Amalow kama msaidizi wake wa masuala ya fedha ili kurejesha mamilioni ya dola zilizokuwa zimewekwa katika akaunti za benki za nje na maafisa kutoka serikali za zamani kwa zaidi ya miaka 21 iliyopita."Uteuzi huu na kuteuliwa kwa Ali Amalow kama afisa kwa dhamana hii kulikuwa jambo makini, chanya na hatua muhimu, lakini rais wa zamani hakushauriana na [tawala za kanda za Puntland na Somaliland] na hakupata mamlaka rasmi kwa suala hili [kwa vile hakuwa rais wa serikali ya kudumua]," alisema Idman Dahir Awale, mtafiti wa masuala ya kifedha wa Somalia.
"Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kuajiri kampuni ya sheria [ya Kimarekani] Shulman Rogers kuwa kama mshauri wa masuala ya sheria na msaidizi kwa aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Somalia," aliiambia Sabahi. Mpango huo uliokuwa na utata ungeipatia kampuni ya Shulman Rogers dola 50,000 na asilimia 3.5 ya mali yoyote ya Somalia au msaada wa fedha waliofanikiwa katika kuupata.
No comments:
Post a Comment