Mwaka 1997, Sophia Abdi Nur alikuwa mwanamke wa kwanza katika jimbo
la Kaskazini Mashariki mwa Kenya kugombea kiti cha siasa wakati
alipogombea uwakilishi wa wilaya ya Ijara katika bunge.
Nur alishindwa katika kinyang'anyiro hicho, lakini aliendeleza kazi
yake kwa ajili ya haki za wanawake na hakutupilia mbali utashi wake wa
siasa. Mwaka 2008, Nur alikuwa mwanamke wa kwanza mbunge kutoka katika
mkoa huo baada ya chama cha Demokrasia cha Orange kumteua katika moja ya
viti vya ubunge 12 vinavyochaguliwa na vyama vya siasa.
Wakati akipiga kampeni kwa kiti cha ubunge cha Ijara kwa mara
nyingine tena katika uchaguzi mkuu wa tarehe 4 Machi, Nur alisema ana
matarajio ya matokeo mazuri kwani baadhi ya changamoto zilizochangia
kushindwa katika jaribio lake la kwanza zimeshughulikiwa.
Nur alizungumza na Sabahi kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake
wanaotafuta majukumu ya uongozi nchini Kenya, hamasa yake, na dira yake
kwa jimbo la uchaguzi la Ijara na jimbo la Kaskazini Mashariki.
Sabahi: Kwa nini ulijiaminisha kwenye siasa za dunia inayomilikiwa na wanaume?
Nur: Nilijiunga na siasa kwa sababu nilitaka kuunyanyua
masuala ya mkoa huu hadi katika ngazi ya taifa na kuhamasisha masuala ya
wanawake. Baadhi ya masuala ya siasa ambayo ni ya muhimu kwenye
maendeleo ya mkoa yanahitaji utashi wa kisiasa.
Niligombea kiti cha jimbo la uchaguzi la Ijara mwaka 1997. Nilikuwa
wa pili nyuma ya Idle Mohamed, kwa kura 2,400 ikilinganishwa na kura
zake 2,500.
Ninaamini kwamba uchaguzi ulikuwa na udanganyifu kwa sababu masanduku
ya kura yalipotea wakati maofisa wawili wa tume ya uchaguzi
walipofariki dunia katika ajali ya barabarani siku ya uchaguzi.
Ningeshinda kama kura za masanduku hayo mawili zingehesabiwa kwa sababu
zilikuwa zimepigwa kwenye maeneo yalioyokuwa ngome yangu.
Baada ya uzoefu huo, nilichukua likizo ya kutokushiriki kikamilifu
katika siasa kwa miaka 10 kwa sababu ya majukumu ya familia na asasi
niliyokuwa ninaindesha kuwasaidia wasichana kuepuka ukeketaji wa
wanawake.
Sabahi: Je, unaweza kulinganisha uzoefu wa kampeni zako za sasa na zile za uchaguzi wa 1997?
Nur: Mwaka 1997, timu yangu ya kampeni ilibidi ipambane na
jamii inayoongozwa kwa kiasi kikubwa na wanaume, ambayo ilikuwa ni
sehemu ya kushindwa kwangu. Baadhi ya wapinzani wangu walitumia mawazo
yasiyobadilika ya kidini na kiutamaduni kwamba mwanamke hafai kuwa
kiongozi. Sikuweza kupiga kampeni hadharani kwa sababu lilikuwa
halijawahi kutokea, hivyo niliwaachia wanaume katika kampeni yangu
kufanya sehemu kubwa ya uhamasishaji.
Jamii yangu ya Kisomali isiyotaka kubadilika iliwakatisha tamaa
wanawake kugombea katika nafasi za uchaguzi katika jimbo. Lakini sasa,
katiba mpya inaturuhusu kutafuta kura kwa uwazi na ninaamini kwamba
elimu ya uraia ya hivi karibuni imeeleweka katika jamii kwa sababu mimi
binafsi ninafanya kampeni kijiji hadi kijiji.
Ninagombea kiti cha ubunge cha Ijara dhidi ya wagombea watano
wanaume. Wote wanafanya kampeni kuhusu masuala mbalimbali na hawatumii
jinsia yangu kunishushia hadhi.
Sabahi: Unajiweka katika nafasi gani ya kuwa mwanamke wa
kwanza kutoka Jimbo la Kaskazini Mashariki kuchaguliwa moja kwa moja
katika bunge?
Nur: Nina matumaini kwamba nitashinda.
Ninaamini katika rekodi yangu ya maendeleo kwa ajili ya jamii kama
sehemu ya WomanKind Kenya. Nilisaidia ujenzi wa shule15 za kati na za
sekondari, na zaidi ya miradi 12 ya maji. Pia nilifadhili vikundi vya
wanawake vya ujasiriamali na kusaidia programu za msaada wa masomo kwa
wasichana 300.
Jamii inathamini kile ambacho nimewafanyia nje ya uongozi wa kisiasa na inaamini ninaweza kufanya zaidi kama nitapewa nafasi.
Sabahi: Ni nini dira yako kwa wananchi wa jimbo la uchaguzi la Ijara na Jimbo la Kaskazini Mashariki kwa ujumla?
Nur: Nitaendelea kujitahidi kuinua hali ya maisha ya wananchi,
kuboresha miundombinu ya mkoa ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi,
huduma za afya, elimu na kutatua historia yake ya ukiukaji wa haki za
binadamu.
Nitatoa kipaumbele katika uhakika wa chakula ili kupunguza vifo vya
mara kwa mara vya watu na mifugo vinavyotokana na ukame. Kutokana na
hilo, nitaanzisha kilimo cha umwagiliaji zaidi.
Sabahi: Unapangaje kufanikisha malengo yako kwa ajili ya mkoa?
Nur: Nitahitaji ushirikiano wa kila mmoja. Nimekuwa nikitafuta
msaada wa wabunge wote kutoka katika mkoa ili tuweze kuzungumza kwa
sauti moja. Nitapatikana kwa urahisi na kukutana na wananchi zaidi.
Nitafanya matumizi ya fedha zilizoletwa kwa busara na kuwajibika kwa
Fedha za Maendeleo ya Majimbo. Nitatafuta pia misaada wa fedha kwa ajili
ya maendeleo na kuhimiza ujasiriamali kushughulikia uwezeshaji wa hali
ya juu.
Sabahi: Nini kinachokusukuma?
Nur: Hali mbaya ya watu wanaohitaji msaada ili kusimama
wenyewe. Hali ya jumla ya kutokuwa na uhakika wa chakula katika eneo
inanifanya mimi kuendelea. Hadi hali ya kudumu ya ukosefu wa chakula
itatuliwe, sitapumzika. Ninajua hali ya kuwa na njaa kwa siku kadhaa na
ninavutiwa na uongozi wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela
ambao haukujali maslahi binafsi.
Sabahi: Je, siku zijazo za wanawake wanashiriki katika siasa ni zipi?
Nur: Katiba mpya imefungua milango kwa wanawake. Japokuwa
zinatenga viti maalumu kwa ajili ya wanawake katika nchi 47 nchini, pia
inatoa nafasi kwa wanawake kuwania nafasi nyingine za uchaguzi.
Sio wote tunaosherehekea kwa sasa, lakini ni hatua ya kwanza kuelekea
mafanikio ya uwakilishi kwa wanawake katika uwanja wa kutawaliwa na
wanaume, hususan katika Jimbo la Kaskazini Mashariki.
Katiba hii inakosoa mila ambayo iliwaweka wanaume juu ya wanawake
katika tabia ya mkubwa kumwonea mdogo na kuzuia nafasi yoyote ya
wanawake kushindana kwa haki katika fani ya elimu, jamii, uchumi na
siasa.
Kikwazo cha msingi kilichobaki ni katika kipengele cha fedha ambacho
kinawapa wanaume wengi kinga. Taratibu kinafikia pazuri, hata kama.
Wanawake katika eneo wanafuatilia maendeleo yangu na matakwa ya Mungu,
kama nitachaguliwa, itatia moyo wanawake wengi kujitokeza.
Wasifu wa Sophia Abdi Nur
Sophia Abdi Nur alizaliwa mwaka 1966 huko Garissa na alisoma katika
Shule ya Msingi ya Modogashe na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jimbo
la Kaskazini Mashariki katika Wilaya ya Garissa. Mwaka 1980, alijiunga
katika Chuo cha Ualimu cha Igoji huko Meru, Jimbo la Mashariki, na baada
ya kumaliza masomo yake alianza kazi yake ya kufundisha katika Shule ya
Msingi ya Young Muslims, Shule ya Sekondari ya Juu ya Wavulana ya Mjini
Garissa na Shule ya Msingi ya Wasichana ya Hyuga.
Nur alipata shahada katika Mafunzo ya Maendeleo katika Kituo cha Mafunzo
ya Maendeleo cha Kimmage huko Ayalandi na shahada ya uzamili katika
utawala na maendeleo ya mashirika katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha
Marekani, Kenya.
Aliacha kufundisha mwaka 1992 na kujihusisha na maendeleo ya jamii. Nur
alianzisha WomanKind Kenya, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha
na shughuli mbalimbali za maendeleo zinazokusudia kuhimiza elimu kwa
wasichana, kuwawezesha wanawake, kampeni dhidi ya vitendo hatarishi vya
kimila kama vile ukeketaji kwa wanawake na masuala mengine ya haki za
binadamu.
No comments:
Post a Comment