Friday, January 18, 2013

Skuli ya Uweleni kisiwani Pemba walia na Uzio


 
 
 
 
 
 
Rate This

 Wanafunzi wakiwa Darasani

UONGOZI wa Skuli ya Sekondari ya Uweleni Mkoani Pemba, umesema unapata hofu na wasiwasi mkubwa wa usalama wa mali za skuli yao, na hasa baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa, iwapo hatua za haraka za kujengewa uzio hazitofanyawa katika kipindi kifupi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Skulini hapo, Mwalimu anaesimamia majenzi Mohamed Ussi, alisema skuli hiyo kwa sasa ina mali nyingi ikiwa ni pamoja na kompyuta, vitabu na mali nyengine, hivyo ni vyema ujenzi huo ukafanywa.

Alisema, kama hilo halitofanyika mapema na hasa kabla ya mafundi waliopo hawajaondoka, watakosa raha kwa vile mali za skuli hazitakuwa na ulinzi wa kutosha kwa vile skuli itakuwa wazi.

Mohamed Ussi alieleza, tayari wao kama uongozi wa skuli hiyo wameshafanya juhudi za kuomba misaada mbali mbali na hata kuiandikia barua Afisi ya Makamu wa pili wa rais  ingawa hadi sasa hilo halijafanikiwa.

Alifafanua kuwa, wameshafanyiwa makisio ya ujenzi wa uzio huo, ambapo jumla ya shilingi laki tano zinahitajika ili kujenga uzio huo ambao wanaamini ukijengwa na kukamilika itakuwa ni kinga kwa skuli hiyo.

‘’Huu uzio kama utajengwa utasaidia pia hata hawa wanafunzi kuwadhibiti maana tutakuwa na mlango  maalum ambao tunautumia, na sio skuli kubwa kama hii kuwa na vichochoro kama kijiji’’,alieleza Mohamed Ussi.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo ya Uweleni Shehe Hassan, alisema kutoka na historia kubwa ya Skuli hiyo, na matengenezo makubwa yaliofanywa haipendezi kuiona haina uzio.

Mwalimu Mkuu huyo alieleza kuwa, wakati umefika sasa kwa wale ambao wanauwezo na wamesoma Skuli hiyo, kuona umuhimu wa kutoa michango yao ya hali mali ili kufanikisha hilo na kuipandisha hadhi skuli hiyo.

‘’Kwa kweli uzio unatukosesha usingizi na sasa hatuna amani na mali za skuli na hata hii inapoteza haiba yake, maana kwa uzuri ilionayo haipendezi kuona haina uzio’’,alifafanua Mwalimu Mkuu huyo.

Katika hatua nyengine uongozi wa hiyo, umeipongeza Serikali kupitia Wizara yake ya Elimu kwa kuamua kuifanyia matengenezo makubwa skuli yao, jambo ambalo limeipandisha haiba skuli hiyo.

Skuli ya Sekondari ya Uwelini iliopo Mkoani Pemba ni moja ya skuli za mwanzo Kisiwani Pemba ambapo kwa sasa Skuli hiyo inaendelea na kufanyiwa matengenezo makubwa na siku chache zijazo itakamilika .

Na Haji Nassor, Pemba

No comments:

Post a Comment