Thursday, January 31, 2013

Umoja wa nchi za Ulaya waahidi kuiongezea misaada Somalia

Viongozi wa Umoja wa nchi za Ulaya hapo siku ya Jumatano (tarehe 30 Januari) waliahidi kuanzisha programu ya kiuchumi na kisiasa kwa ajili ya Somalia wakati wa ziara ya Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia mjini Brussels, kikiwa kituo cha mwanzo katika ziara yake ya Ulaya, liliripoti shirika la habari la AFP.
Mkuu wa sera za nje wa umoja huo, Catherine Ashton, alitangaza kwamba Umoja wa nchi za Ulaya utafanya mkutano wa kimataifa katika majira ya demani kwa ajili ya "kupatikana kwa Mpango Mpya kwa Somalia ambao utasaidia kutoa uungaji mkono wa kisiasa, kiusalama na kimaendeleo."
Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, alisema kwamba pande zote zilikubaliana kuimarisha mahusiano ya Umoja huo na Somalia. "Tunaamini kuna dhamira ya dhati ya kusonga mbele," alisema.
Umoja wa nchi za Ulaya umechangia euro milioni 600 (dola milioni 814) kwa Somalia ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita ikiwa ni sehemu ya mpango wenye maeneo matatu ya usalama, diplomasia na maendeleo.
Mohamud alisema taifa lake linahitaji msaada mkubwa ili lihame kutoka nchi "yenye kupata ahuweni" kuwa nchi inayojijenga tena. "Kila kitu kiko sifuri, kila kitu kinapaswa kuanza mwanzo kabisa," alisema. "Na hatuwezi kufanya hilo peke yetu."
Mohamud amepangiwa kukutana na mawazi wa kigeni wa mataifa 27 ya Umoja wa nchi za Ulaya siku ya Alhamisi kabla ya kuelekea London.

No comments:

Post a Comment