Kampeni hiyo ilianza tarehe 26 Januari na itaendelea kwa wiki moja, au zaidi kama itahitajika, ili kupendezesha na kusafisha wilaya zote 16 za mkoa wa Benadir.
Wanaojitolea wanasema hawahitaji malipo kwa kazi hiyo, lakini ili kuifanya shughuli inoge zaidi, serikali ya shirikisho inatoa zawadi za fedha taslimu kwa wilaya ambazo zitapiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo katika usafishaji.
"Nitazizawadia wilaya ambazo zitapata alama tatu za mwanzo katika kampeni ya usafishaji ya Mogadishu," alisema Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon hapo tarehe 21 Januari. "Wilaya itakayoshinda itapata dola 15,000, wilaya ya pili itapata dola 10,000 na wilaya ya tatu itapata dola 5,000."
Serikali ya shirikisho bado haijatoa vigezo vya kuwachagua washindi wakati kampeni hiyo itakapomalizika siku ya Ijumaa (tarehe 1 Februari), au ikiwa itahitaji wilaya zitakazoshinda zitumie fedha hizo kwa miradi mahsusi.
Mkurugenzi wa idara ya usafi ya Benadir, Hussein Warsame Abtidon, alisema operesheni za usafishaji zinaendelea vyema hadi sasa, huku kukiwa na watu wanaojitolea wafikao 200 ambao wanashiriki katika kila wilaya.
"Tunataka kumaliza kampeni ya usafishaji wiki hii, lakini muda utaongezwa ikiwa itakuwa lazima ili kuifanya Mogadishu kuwa mji safi na wenye siha," aliiambia Sabahi.
Abtidon alisema kampeni italeta tofauti kubwa katika hali ya usafi mjini Mogadishu na kwamba ana matumaini kuwa itarejesha uzuri wa mji siku za neema.
Wilaya zashindania zawadi ya juu kabisa
Omar Abdulle Osman, msimamizi katika wilaya ya Hilwa, alisema usafishaji unaendelea vyema katika eneo lake."Mimi nina matumaini kwamba wilaya yangu itashinda kwa sababu tunafanya juhudi kubwa sana ili kuboresha hali ya usafi katika wilaya ya Hilwa," aliiambia Sabahi. "Ikiwa tutashinda mashindano haya, ninawaahidi watu wanaojitolea kuwa watapata fursa ya kuamua pesa hizo zitumike kwa ajili gani."
Deqa Abdikadir, msimamizi katika wilaya ya Warta Nabada, ambayo hapo kabla ilijulikana kama Wardhigley, alisema watu 200 wa kujitolea wanaosafisha wilayani kwake hawatarajii malipo yoyote kwa juhudi zao. Hata hivyo, yeye ana matumaini kuwa watashinda.
"Nina matumaini makubwa kwamba wilaya ya Warta Nabada itapata nafasi ya kwanza katika kampeni za wiki moja za mashindano ya usafishaji Mogadishu," alisema. "Tutafanya kazi ngumu ili tushinde."
Watu wanaojitolea, wanawake na wanaume wanashiriki katika kampeni za wiki moja walichaguliwa na kupendekezwa na wazee katika kila kitongoji, kwa mujibu wa wasimamizi wa wilaya. Wanaojitolea hao hufanyakazi kutoka saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana na hupelekwa kila kitongoji katika timu za watu 15 hadi 20.
Osman Abdi, mwenye umri wa miaka 36 na anayejitolea, alisema kuwa anataka awe sehemu ya juhudi za kurejesha usafi katika mji wa Mogadishu, hasa katika wilaya ya Warta Nabada ambako anaishi.
"Hakuna mtu anayetulipa kwa operesheni za usafishaji tunazofanya," aliiambia Sabahi. "Tunataka kuisafisha wilaya yetu ili kuboresha maisha yetu kwa sababu kuna msemo usemao, 'magonjwa hayakai mbali na takataka'."
Dk. Ahmed Mohamed Sheikh, mtaalamu wa afya ya umma, alisema kuwa kampeni ya usafi ni ndogo lakini ni mwanzo muhimu sana kwa ajili ya mji.
Alisema kuwa Mogadishu inahitaji kampeni za usafi za muda mrefu zaidi kwani hakuna mtu ambaye amejaribu kuusafisha kwa zaidi ya miaka 20. "Wiki moja haitoshi kuisafisha Mogadishu na lazima ipangiwe kusafishwa mara kwa mara," aliiambia Sabahi.
"Naamini kwamba changamoto yetu kubwa ni hali mbaya ya uchafu ya nchi nzima," alisema. "Tunatarajia kuwa utawala mpya utalishughulikia tatizo hilo."
No comments:
Post a Comment