Tuesday, January 15, 2013

Wajumbe kadhaa wakutana kujadili mambo yanayohusu Muungano

 
 
 
 
 
 
Rate This


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifafanua hatua zinazoendelea kuchukuliwa  katika suala la mafuta na gesi kutolewa katika mambo ya Muungano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifafanua hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika suala la mafuta na gesi kutolewa katika mambo ya Muungano.

Wajumbe wa Kamati ya pamoja kati Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  wamekutana katika utaratibu wao wa  kawaida wa kujadili masuala yanayohusu  Muungano.
Kikao hicho ambacho kilikuwa  chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal na kushirikisha Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi,Mawaziri wa SMT,SMZ na baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali zote mbili kilifanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort  Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Wajumbe wa Kikao hicho walipitia na kuridhia kumbukumbu za Kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Tarehe 28 Januari mwaka 2012 Mjini Dar es salaam pamoja na kupokea Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Aidha wajumbe hao walipitia na kuridhia mapendekezo kuhusu utaratibu wa muda wa mgao wa ajira kwa Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kupitia    makubaliano ya hoja zilizopatiwa ufumbuzi.
Wakichangia Hoja mbali mbali zilizowasilishwa kwenye Mkutano huo baadhi ya Wajumbe wa Kikao hicho wameelezea kuridhika kwao na hatua zinazochukuliwa na  Ofisi ya Waziri Mkuu na ile  ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini ya usimamizi wa Wanasheria Wakuu wa Pande zote mbili katika kulishughulikia suala la mafuta na gesi kuondolewa katika mambo ya Muungano.
Walisema hatua ya  kuridhiwa na kukubaliwa na Maraisi  wa Serikali zote mbili Nchini  limewawezesha na kuwapa nguvu wataalamu wa sheria wa pande zote mbili kuangalia namna ya kuandaa utaratibu utakachokidhi mahitaji ya kisheria ya kila upande kuhusu suala hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alisema mwenendo mzima wa utekelezaji wa masuala yanayoleta kero ndani ya Muungano unakwenda vyema kufuatia mfumo wa vikao vinavyohusisha watendaji wa pande zote mbili.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohd Gharib Bilal akikiendesha Kikao cha pamoja cha SMT na SMZ akiwa Mwenyekiti hapo Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohd Gharib Bilal akikiendesha Kikao cha pamoja cha SMT na SMZ akiwa Mwenyekiti hapo Zanzibar Beach Resort Mbweni.

Waziri Samia alisema hata hivyo yapo baadhi ya masuala  ambayo huchukuwa muda mrefu kuyapatia ufumbuzi kutokana na mfumo wa sheria unaohitaji mabadiliko ili kwenda sambamba na makubaliano yaliyoridhiwa.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo  Pinda akitoa shukrani zake aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maadhimisho mazuri ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Mwaka huu zilizokuwa za mfano wa aina yake.
Mh. Pinda alisema jamii ingependa kuona sherehe za Mapinduzi za Mwakani kutimia nusu karne zikawa za mafanikio makubwa zaidi na Serikali ya Muungano wa Tanzania inaandaa fikra ya namna ya kuongeza nguvu za ushiriki na mchango wake katika kufanikisha sherehe hizo.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema umahiri wa Mawaziri wa Pande zote mbili katika kikao chao cha sekreterieti umewezesha kamati ya pamoja ya SMT na SMZ  kufanikiwa kwa hali ya juu.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wajumbe wa kikao hicho wameweza kupokea na kuridhia masuala mbali mbali waliyoyaagiza katika kikao cha mwaka jana  ambayo yalikuwa yakileta kero katika masuala ya Muungano.
Akikifunga kIkao Hicho Mwenyekiti wa Kamati ya pamoja na Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Mohd Gharib Bilal alishauri Viongozi  wa Wizara za  Serikali zote mbili kuendelea kushirikiana ili kuleta ufanisi zaidi.
Dr. Bilal alisema ushirikiano huo utakaoshirikisha pia watendaji na wataalamu wa sekta husika ndani ya taasisi zao utasaidia kupunguza na hatimae kuondosha kabisa  kero zinazosababisha hitilafu ndani ya mfumo wa Muungano.
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ kilichofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ kilichofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Masuala yaliyowasilisha  katika kikao hicho cha Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ  na kupokewa na kuridhiwa na wajumbe hao ni pamoja na uwezo wa SMZ kukopa nje ya Nchi, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, kodi ya mapato-pay as you earn { PAYE} pamoja na suala la Mafuta  la kutaka kutolewa katika mambo ya Muungano.
Kikao kijacho cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kinatarajiwa kufanyika mara baada ya Sherehe za mwaka huu za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kufanyika pahali zitakapofanyika Sherehe hizo.

No comments:

Post a Comment