Wednesday, January 30, 2013

Wakimbizi wa Somalia nchini Kenya wailalamikia serikali kwa kuweka msukomo wa uhamisho wa makaazi

Abdiweli Bulle mwenye umri wa miaka themanini anahofia kuhusu maelekezo ya hivi karibuni ya serikali ya Kenya ambayo inataka wakimbizi kurudi kwenye makambi kwamba kutaharibu maisha aliyojijengea huko Nairobi kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Bulle na maelefu ya Wasomali walikosa makaazi kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilianza mwaka 1991 baada ya kuanguka kwa serikali kuu ya Somalia. Bulle na familia yake ya watu watano walikimbilia Kismayo wakati vurugu zilipofika Marka, mji wake aliozaliwa. "Mwaka mmoja baadae, hatukuweza kuvumilia vurugu zilizoongezeka na tulilazimika kukimbia tena, tukafika kwenye kambi mchanganyiko ya Dadaab nchini Kenya," Bulle alisema.
Baada ya serikali kuipa idhini familia yake kuwa na hadhi ya wakimbizi , aliondoka kambini mwaka 1994 akiwa kwenye lori la mifugo na kuelekea Nairobi kutafuta fursa za ajira. "Mimi na rafiki yangu tulichagua Eastleigh kuwa mwisho wa safari yetu, na kutokea hapo kumekuwa nyumbani kwetu," alisema.
Alipata kazi mara moja kama mpandisha mizigo kwenye lori na kutumia fedha anazopata kununulia chakula, ambacho alianza kukiuza kando ya barabara huko Eastleigh. Hatimaye Bulle aliileta familia yake kutoka Dadaab na anaelekea kuwa msambazaji mkuu wa vyakula, akiajiri watu zaidi ya 30 katika maeneo manne.
Bulle alisema angeweza kupoteza kila kitu alichojipatia kama serikali itamlazimisha kurudi Dadaab, na anaweza tena kuanza kutegemea misaada.

Kuhamishwa tena wakimbizi kunamaanisha kuimarisha usalama

Tarehe 18 Desemba, Wizara ya Nchi inayoshungulikia Uhamiaji na Usajili wa Watu iliagiza wakimbizi wote katika maeneo ya mjini kurudi katika makambi ya wakimbizi yaliyoteuliwa. Wakimbizi wa Kisomali wanatarajiwa kuripoti maeneo ya wakimbizi ya Dadaab na wale kutoka katika nchi nyingine wanatakiwa kuripoti katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma.
Wizara ilisimamisha mara moja kupokea na kuandikisha wakimbizi katika maeneo ya mjini.
"Tulilazimishwa kufanya uamuzi huu kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi," alisema kaimu kamishna wa Idara ya Mambo ya Wakimbizi Sora Badu Katelo. "Tusifikiriwe vibaya wala sio ubaguzi kwa namna yoyote, bali inamaanisha kuwalinda raia wetu na nchi kutokana na vitisho vya kutokuwa na usalama na mashambulizi yanayofanywa na al-Shabaab na wanaowaonea huruma, ambao wanajifanya kuwa ni wakimbizi."
Katelo aliiambia Sabahi kwamba kuwaweka wakimbizi katika kambi itarahisisha vikosi vya usalama kufuatilia vitendo vya uhalifu.
Alisema wakimbizi ambao hawataondoka katika maeneo ya mijini kwa hiyari yao, wataondolewa kwa nguvu, lakini alikiri kwamba serikali bado haijaja na mpango wa kushughulikia kesi kwa wakimbizi wanaomiliki mali au wenye vitegauchumi.
Serikali imepanga tarehe 21 Januari kama tarehe ya mwisho ya kuhama kwa hiyari, na baada ya hapo wakimbizi watahamishwa kwa nguvu. Hata hivyo, wiki iliyopita, Mahakama Kuu ya Kenya ilisimamisha uamuzi kwa muda kuhamisha wakimbizi wakati mahakama ikisikiliza kesi dhidi ya tukio hilo.

'Pahali pekee ninapopajua na kupaita nyumbani ni Eastleigh'

Hassan Abshir, ambaye anauza nguo katika soko la ndani na mazulia yaliyotoka nje, alisema aliwasili katika eneo la Dadaab mwaka 1991 alipokuwa na umri wa miaka 16.
"Tulikuwa miongoni mwa wakimbizi wa mwanzo kusajiliwa kambini, lakini siku moja mama yangu akaugua. Hii ilitulazimisha kuja Nairobi ili kupata matibabu katika Hospitali ya Tafa ya Kenyatta," aliiambia Sabahi.
Tulipofika, familia yangu ikaa Eastleigh pamoja na rafiki wa mama yake Abshir, ambaye wakati huo alitupatia mtaji wa kuanzisha biashara.
"Pahali pekee ninapopajua na kupaita nyumbani ni Eastleigh, na hatutakubali kurejeshwa iwe Dadaab au Somalia," alisema.

Kulazimishwa kuhama kunakiuka haki za wakimbizi

Rufus Karanja, afisa mipango wa Muungano wa Wakimbizi wa Kenya, ambao hutoa msaada wa kisheria kwa watu wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi, alisema kuwa uamuzi wa serikali unakiuka haki za wakimbizi na ni kinyume na majukumu ya Kenya kimataifa.
"Tumewasiliana na serikali katika suala hili mara nyingi, na maafisa wameshindwa kutuonesha ni vipi wakimbizi katika vituo vya mijini ni tishio kwa usalama wa taifa na wafute uamuzi wao wa kuwataka warejee makambini," Karanja aliiambia Sabahi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi ya mwaka 2006, alisema, wakimbizi wanayo haki kukaa popote nchini ilimradi tu wanazo nyaraka zinazofaa za kuthibitisha hadhi yao.
Alisema wakimbizi wengi walilazimika kuondoka makambini kutokana na hali mbaya za maisha, kujazana, na ukosefu wa huduma na vitu vya msingi kama vile hospitali na shule. Kwa kuja mijini, wakimbizi wameweza kujitegemea na kuachana na misaada, kujijumuisha na maisha ya kijamii na kiuchumi kwa kuanzisha biashara au kufanyakazi kama vibarua, alisema.
"Kuwalazimisha kurejea makamabini ni kama kukebehi ujasiri wao na kutafuta kwao mafanikio na kuachana na tabia mbaya," alisema. "Hii inawaumiza na tutaipinga serikali mahakamani ili kulinda haki za wakimbizi."
Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, ambalo limelaani uamuzi wa Kenya wa kukata huduma kwa wakimbizi katika maeneo ya mijini, zaidi ya wakimbizi 54,000 wanaishi mjini Nairobi.
Kuwarejesha wakimbizi wengi kiasi hicho kwenda Dadaab kutazidisha shinikizo makambini, kambi ambazo tayari zimezidiwa, Karanja alisema, na kuongeza kuwa hili litapelekea mizozo zaidi na hali ya kutokuwepo utulivu.

No comments:

Post a Comment