Monday, January 7, 2013

Wateja wa simu za mkononi wapata teknolojia ya 3G mjini Mogadishu

Kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Hormuud Telecom Somalia imepanua huduma zake za kizazi cha tatu (3G) za mtandao wa simu za mkononi mjini Mogadishu ili kutoa upatikanaji wa intaneti ya kasi kwa wateja wanaotumia simu na kompyuta za mkononi zenye uwezo wa kunasa intaneti.
  • Ofisi yahuduma kwa wateja ya kampuni ya The Hormuud Telecom mjini Mogadishu ikiwa imefurika wateja siku moja hivi karibuni. [Faili/Sabahi]
  • Modem za USB zinaziwezesha kompyuta kunasa intaneti kwa kutumia mtandao wa 3G wa Hormuud. [Na File/Sabahi]
Huduma hiyo mwanzoni ilikuwa inapatikana katika baadhi ya maeneo tu kaskazini ya Somalia, lakini kwa mara ya kwanza kampuni inaanzisha huduma hizo kwa nchi nzima. Mtandao wa 3G wa Hormuud mwanzo utapatikana mjini Mogadishu na utaenea kwenye miji mengine ya kusini mwa Somalia ndani ya mwaka mmoja.
Kwa Somalia, ambayo mwaka 2000 ilikuwa moja kati ya mataifa ya mwisho kabisa barani Afrika kujiunga na intaneti, haya ni maendedeleo makubwa.
Akitangaza huduma hizo katika Shamo Hotel hapo tarehe 29 Disemba, mwenyekiti wa Hormuud, Ahmed Mohamud Yusuf, alizungumzia kuhusu umuhimu wa teknolojia mpya kwa jamii. "Huduma hii mpya itatoa intaneti ya kasi kubwa ambayo itawasaidia wanafunzi kujifunza, wasomi kufanya utafiti na umma mzima kuungana na dunia kwa kupitia jukwaa la vyombo vya habari," alisema.
Naye mkurugenzi masoko wa Hormuud Abdihakim Hassan Idow alisema kuwa zaidi ya wateja 150,000 mjini Mogadishu wameshajiunga na huduma za 3G, ambayo inatoa upatikanaji wa vifaa vya mkononi vinavyorusha matangazo ya kusikia na video, kuzungumza kwa kutumia video na usafirishaji wa data kwa kasi kubwa.
Hormuud ilikuwa kampuni ya kwanza kutoa huduma za upatikanaji wa intaneti mwaka 2011, na kuingizwa kwa huduma za 3G kunatoa upatikanaji wa haraka zaidi na kuboresha teknolojia iliyokuwepo kabla.
"Kampuni yetu inatoa huduma kwa wateja zikiwa ni pamoja na kutuma fedha kwa kutumia simu na modem za USB kwa upatikanaji mpana wa itaneti katika nchi fulani za Kiafrika na Kiarabu," Idow aliiambia Sabahi. "Tuanatarajia kuwa huduma hii itakidhi mahitaji makubwa ya upatikanaji wa intaneti kwa wanafunzi, waandishi wa habari, wizara, wakala wa misaada, asasi za tiba, vyuo vikuu, kampuni binafsi, maofisi na kwa ajili ya mikutano [sehemu za kufanyia]."
Idow alisema kuwa kampuni ya Hormuud inuza modem za USB kwa bei ya kiasi cha dola 50, ambazo bado zinaweza kuwa ni bei ya juu kwa Wasomali, ambao wanatumia intaneti kwa kasi inayokua.
Alisema kuwa idadi ya watu waliojiandikisha na 3G inaendelea kupanda na anatarajia kuwa hatimaye teknolojia itatawala soko la ndani.
"Teknolojia ya 3G ina kasi zaidi kuliko ADSL na ndio pekee inayoruhusu kupatikana kwa intaneti mahali popote kwa kutumia mtandao wa kutembea na intaneti, na kufanya kuwa ndio chaguo pekee kwa wale walioko mbioni mara zote," alisema. ADSL, hutoa upatikanaji wa intaneti kwa kutumia njia ya simu.

Soko la intaneti la Somalia

Mwanauchumi Samira Mohamed Waeys alisema kuwa soko la intaneti la Somalia limekabiliwa na ushindani miongoni mwa makampuni ya simu za mkononi, ikiwa ni pamoja na kampuni za Telesom, SomTel, Golis, Telecom Somalia, NationLink Somalia, Global Internet Company na Hormuud Telecom.
Waeys aliiambia Sabahi kuwa kuanzishwa kwa huduma za 3G kunawawezesha watumiaji mjini Mogadishu kuvinjari katika tovuti kwa kasi kubwa kama vile megabaiti moja kwa sekunde katika jiji na viunga vyake. Huduma za kasi zaidi zitaboresha utiririkaji wa habari jijini na kulifungua jiji kwa dunia, alisema.
Farhan Ahmed Abdullahi, mtaalamu wa teknolojia ya habari, alisema licha ya maendeleo ya 3G, bado Somalia iko nyuma ya wakati, wakati makampuni ya simu Ulaya na Japani wanajaribu teknolojia ya kizazi cha nne (4G). Wakati 3G inaaweza kusafirisha data kwa megabaiti nyingi kwa sekunde, 4G inaweza kufikia gigabaiti 1 kwa sekunde.
"Somalia itajirudi na kuendelea licha ya matatizo kama vile vurugu, mapigano ya ndani ya hasara zitokanazo na ugaidi, ambazo zimeharibu miundombinu ya nchi," aliiambia Sabahi. Kupanuliwa kwa huduma za 3G na kampuni ya Hormuud, ambayo sasa ina watumiaji wa msingi milioni 5, kunaonyesha uwezo wa Somalia kujiweka sawa haraka na matumizi ya teknolojia mpya, alisema.
Mariam Amine Ahmed, mwandishi wa habari mstaafu, alisema kuwa kuingizwa kwa upatikanaji wa simu bila ya kutumia waya kunaweza kuwahamasisha watoaji wa huduma za intaneti kwa laini za simu kupunguza bei zao na kubaki kuwa washindani.
"Intaneti imepenya kwenye maeneo yote ya maisha yetu," aliiambia Sabahi. "Kwa sababu hii, tunatoa wito kwa watoa huduma wanaoshindana kushusha gharama za upatikanaji wa intaneti kwa njia ya ardhini na bila waya, hasa kwa vile 3G imeingia katika soko la intaneti inayotumia laini za simu."

No comments:

Post a Comment