Monday, January 7, 2013

9 wafa, 12 wapotea baada ya boti kuzama Ziwa Tanganyika

Watu tisa wamekufa na wengine 12 kupotea baada ya boti kuzama alfajiri ya siku ya Ijumaa (tarehe 4 Januari) katika Ziwa Tanganyika mkoani Rukwa magharibi mwa Tanzania, mamlaka zilisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma Fraiser Kashai aliiambia Sabahi kwamba boti hiyo ilizama kwa sababu ya upepo mkali. Ilikuwa imebeba abiria 85 na pia tani kadhaa za dagaa, mboga na bidhaa nyengine.
Kashai alisema boti hiyo iliyokuwa ikitokea bandari ya Kirando ikiwa safarini kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ilizama kabla ya kufikia Burundi. Alisema matumaini ya kuwapata abiria walio hai yanatoweka kila muda unapopita.
Msemaji wa polisi Advera Senso aliliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kwamba watu 60 waliokolewa.
Mwandishi wa habari aliyepo Kigoma, Anthony Kayanda, alisema idadi ya waliokufa inaweza kuwa kubwa zaidi kwani kuna uwezakano mkubwa kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba abiria wasiosajiliwa.
“Waliookoka wanasema idadi ya watu kwenye boti ilikuwa zaidi (ya abiria 85),” alisema. “Wanasema hakukuchukuliwa rikodi yoyote wakati wa kupanda chombo. Ilhali uwezo wa boti ni abiria 70 tu, kawaida huchukua hadi abiria 120.”
Kayanda alisema taarifa kuhusiana na ajali hiyo zilichelewa kwa sababu hakukuwa na mitandao ya simu za mkononi kwenye eneo hilo. Polisi wanashirikiana na raia kuwaokoa abiria, alisema.

No comments:

Post a Comment