Imewekwa na Hamed Mazrouy

Mwakilishi
wa Jimbo la Kwamtipura Mh.Hamza Hassan Juma akipokea msaada wa Vitanda
12 kwa ajili ya Hospitali ya Jimbo la Kamtipura ili kuongezewa nguvu ya
utoaji huduma Hospitali hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi msaada wa Vitanda 14 na
Magodoro Matano kwa ajili ya Hospitali ya Kwamtipura ili kuiongezea
nguvu ya ziada katika kutoa huduma za Afya kwa Wananachi.
Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi pia
akakabidhi Mifuko 20 ya Saruji kwa uendelezaji wa ujenzi wa Matawi ya
Chama cha Mapinduzi ndani ya Jimbo la Kwamtipura.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alikabidhi msaada huo hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo
ya Mji wa Zanzibar hafla ambayo pia ilishuhudiwa na Baadhi ya Viongozi
na wanachama wa chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Kwamtipura.
Akikabidhi msaada huo kwa
Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma Balozi Seif
alielezea kutiwa moyo na Juhudi za Uongozi na Wananchi wa Jimbo hilo za
kujiletea Maendeleo sambamba na kuimarisha Ustawi wa Jamii.
Alisema Hospitali ya Kwamtipura
inastahiki kupewa msukumo wa kupatiwa vifaa kutokana na mazingira ya
ukubwa na ubora wake unaoendelea kusaidia wananchi sio wa Jimbo hilo
bali hata wa majimbo mengine Jirani.
“ Kwenye ziara yangu ya
kutembelea Taasisi za Wizara ya Afya mwaka uliopita nikiwa Hospitali ya
Kwamtipura niliushauri Uongozi wa Wizara hiyo kuangalia utaratibu wa
Kuitumia Hospitali hiyo kama Tawi la Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja. Na
kwa Taarifa za karibuni suala hilo limekuwa likifanyiwa kazi na Uongozi
huo” Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia uhai wa Chama cha
Mapinduzi Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM aliutaka uongozi wa Jimbo hilo kuhakikisha kwamba
chama hicho kinaendelea kupewa nguvu kwa lengo la kukiwezesha kufanya
vyema katika utekelezaji wa ilani yake iliyonadiwa wakati wa Uchaguzi
Mkuu na kupata ridhaa ya Wananachi walio wengi Nchini.
Akipokea msaada huo Mwakilishi wa
Jimbo la Kwamtipura Mh. Hamza Hassan Juma alimshukuru Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kwa juhudi zake anazoendelea kuchukuwa za kuunga
mkono nguvu za Wananachi katika miradi tofauti ya Kiuchumi na Ustawi wa
Jamii.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi
akimkabidhi mifuko 20 ya Saruji Mwakilishi wa Jimbo la Kwmtipura Mh.
Hamza Hassan Juma kwa ajili ya uendelezaji ujenzi wa Matawi ya Chama
hicho yaliyomo ndani ya Jimbo hilo.
Mh. Hamza alimuhakikishia Balozi
Seif kwamba Uongozi wa Jimbo hilo utahakikisha kwamba Jimbo hilo
linatarajiwa kukabidhiwa tena kwa Chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi
Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Naye Katibu wa Chama cha
Mapinduzi Jimbo la Kwamtipura Bibi Stumai Mohd Mshimbe alisema msaada wa
Balozi Seif utaongeza ari na nguvu kazi kwa Wanachama hao katika
kujisogeza zaidi kwenye maendeleo ya chama chao.
Msaada huo wa Vitanda 12,
Magororo Matano pamoja na Saruji Mifuko 20 umegharimu jumla ya Shilingi
MilioniTatu na Laki Tisa { 3,900,000- }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/2/2013.

No comments:
Post a Comment