Imewekwa na Mhamemed khamis
Mkurugenzi
wa Idara ya Vitambulisho Zanzibar (Zan ID), Mohd Juma Ame akionesha
mfumo wa utayarishaji wa vitambulisho hivyo katika ofisi hizo zilizoko
Mazizini Zanzibar. (Picha na Salmin Said, OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea umuhimu wa kuwepo uadilifu
katika mchakato mzima wa utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi.
Amesema kitambulisho hicho ni
muhimu kwa maendeleo na usalama wa taifa, hivyo umakini na uadilifu
unahitajika kuhakikisha kuwa wanapewa wanaohusika.
Maalim Seif ameeleza hayo leo
wakati akiwa katika ziara maalum ya kutembelea ofisi za usajili na kadi
za utambulisho Zanzibar pamoja na kituo cha Serikali Mtandao
e-government kilichopo Mazizini.
Amesema kuna taarifa kuwa wapo
baadhi ya watu wasiokuwa raia wa Tanzania wamekuwa wakipatiwa
vitambulisho hivyo na kuwaacha wazanzibari wenye sifa, jambo ambalo ni
hatari kwa usalama wa nchi.
Hata hivyo ameelezea
kuridhishwa kwake na utendaji wa ofisi hiyo, na kuwataka kuongeza juhudi
ili kuhakikisha kuwa wanapata ujuzi wa kutosha katika kuendeleza kazi
hiyo.
Amewahimiza wanasiasa
kuwashajiisha wafuasi wao kufuatilia vitambulisho vyao, ili kila
mzanzibari aliyetimiza masharti aweze kupata kitambulisho hicho ambacho
kitamsaidia katika harakati zake za maisha.
“Kitambulisho hiki ndio maisha
kwa sasa, bila ya kuwa nacho huwezi kufanya jambo lolote la maendeleo,
yaani hata ukitaka leseni ya udereva lazima uwe na kitambulisho, seuze
kusafiri, kuendelea na masomo au kutafuta ajira”, alifahamisha Maalim
Seif.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Idara ya Vitambulisho Bw. Mohd Juma Ame amemuhakikishia Makamu wa Kwanza
wa Rais kuwa wanafanya kazi kwa utaalamu wa hali ya juu kuhakikisha
kuwa hakuna udanganyifu unaofanywa katika utoaji wa vitambulisho hivyo.
Maalim
Seif akiangalia ramani ya Zanzibar jinsi Mkonga wa Mawasiliano
unavyoweza kuziunganisha taasisi za serikali kupitia mradi wa
e-government katika ofisi za kituo hicho Mazizini Zanzibar.
Amesifu ubora wa vitambulisho
vya Mzanzibari Mkaazi, na kwamba vinatengenezwa kwa kutumia teknolojia
ya hali ya juu inayoweza kudhibiti taarifa za siri za muhusika ambazo
haziwezi kuonekana bila ya kutumia kifaa maalum, na hivyo kuweza
kudhibiti ubadhirifu.
Akizungumzia kuhusu mtandao wa serikali, e-government Maalim Seif
amesema mradi huo umeanza vizuri na kutaka undelezwe kwa maslahi ya
taifa.
Ameelezea matumaini yake kuwa
iwapo mpango huo utatumiwa vizuri unaweza kupunguza gharama za
uendeshaji wa serikali, kwa vile watendaji wataweza kuwasiliana, kufanya
vikao na kukubaliana kupitia njia hiyo ya mtandao.
Amewahimiza watendaji wa ofisi
hiyo kuandaa vipindi maalum vya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa
mfumo huo wa e-governmet, ili kuongeza uelewa na kuweza kuona faida za
mfumo huo
No comments:
Post a Comment