
Feb
4
2013
Imewekwa na Hamed Mazrouy
ASKARI wa Idara ya Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya
Biharamulo mkoani Kagera, wamechoma moto na kuharibu nyumba za familia
zaidi ya 200 katika kijiji cha Namalandula kata ya Namonge wilayani
Bukombe mkoani Geita.
Katika tukio hilo wananchi wa kijiji hicho wakiongozwa na Diwani wao,
Patrick Kaburusi walisema askari hao waliingia kijijini hapo juzi na
kuanza kuwashambulia na kuwafukuza kwa kupiga risasi hewani wakiwatuhumu
kuishi kwenye hifadhi ya halmashauri hiyo kinyume cha sheria.
Diwani wa kata hiyo iliyopo mpakani mwa Wilaya ya Biharamulo na
Bukombe, alisema pamoja na askari hao kuendesha Operesheni ya wiki mbili
ya kuwaondoa wavamizi wa maeneo ya hifadhi, kijiji hicho hakihusiki na
uvamizi huo kwani kiko kihalali na wananchi wake wameishi kwa siku
nyingi katika maeneo hayo.
Alisema wananchi hao waliingia katika maeneo hayo kwa kununua kutoka
Serikali ya kijiji ambayo iliwapimia kupitia kamati yake ya ugawaji wa
ardhi na kuongeza kuwa ni hali ya kushangaza kuona askari hao
wanawafanyia unyama wa kuwaondoa kwa nguvu katika maeneo hayo.
Kufuatia hali hiyo wananchi hao pamoja na familia zao hawana mahala
pa kuishi baada ya makazi yao kuchomwa moto na mengine kuharibiwa na
askari hao kutoka wilayani Biharamulo mkoani Kagera wakidai walikuwa
wakiishi kwenye eneo la hifadhi ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo,Richard Mbeho alisema
operesheni hiyo ina lengo la kuwaondoa wavamizi haramu wa maeneo ya
Serikali ambao waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa ulaghai wa viongozi wa
Serikali ya kijiji hicho ambao walikuwa wakiwauzia.
Imedaiwa kuwa wananchi hao waliingia kwenye eneo hilo kwa kuuziwa na
viongozi wa Serikali ya kijiji cha Namalandula kwa gharama ya kati ya
Sh1 hadi Sh2 milioni kwa eneo lenye ukubwa wa hekari moja au mbili na
wameishi kwa kipindi kirefu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenigoha alisema suala hilo
analo na analifanyia kazi kwa kuwasiliana na viongozi wa Wilaya ya
Biharamulo ili kuona mipaka ya hifadhi hiyo na kijiji cha Namalandula
kinachodaiwa kuwa ndani ya hifadhi hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya aliyeongea kwa njia ya simu kutoka Dodoma
alisema mara tu atakaporejea wilayani kwake atalishughulikia suala hilo
ikiwa ni pamoja na kwenda kuwaona wananchi hao wanaodaiwa kuishi
msituni bila kuwa na nyumba za kuishi.
No comments:
Post a Comment