MTOTO mchanga wa siku 21 ameokotwa akiwa hai katika maeneo ya Chanika, jijini Dar es Salaam, baada ya kutupwa na mtu asiyefahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Komba, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 6:00 usiku wakati askari wakifanya doria.
Alisema kuwa mtoto huyo amehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili huku afya yake ikiendelea vizuri na juhudi za kumtafuta aliyemtupa zinaendelea.
Katika tukio lingine, watu watatu wamefariki akiwemo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Navy Kigamboni katika ajali iliyohusisha gari na pikipiki kugongana katika maeneo tofauti hapa jijini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiyondo, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi katika barabara ya Kibada na Ferry eneo la Chuo cha Wakorea.
Alisema kuwa gari yenye namba za usajili T 740 AMJ aina ya Scania ikiwa na Trailler T 687 AZL ikiendeshwa na Masoud Hemed (45) mkazi wa Kibamba akitokea Kibada kuelekea Ferry, aligongana na pikipiki yenye namba za usajili T 401 BRC aina ya Toyo ikiendeshwa na askari wa JWTZ kikosi cha Navy Kigamboni, Edmund Batholomeo (55).
Kiyondo alisema askari huyo alikuwa amembeba abiria aliyetambuliwa kwa jina la Anastasia Edmund (22) mkazi wa Kisiwani na kuwa katika muelekeo mmoja na dereva wa gari.
Wakati huohuo, mwendesha pikipiki na mfanyakazi wa Dawasco mtambo wa Ruvu Chini, Fidelis Baita (35-40), amefariki baada ya kugongwa na gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 4:00 usiku katika barabara ya Bagamoyo eneo la IMTU.
No comments:
Post a Comment