Tuesday, February 12, 2013

PEMBA WATAKIWA KUTHAMINI JUHUDI BINAFSI ZINAZOTOLEWA KWA MIFUGO

 
 
 
 
 
 
Rate This

NA: Ali Khamis,Pemba.
JAMII imetakiwa kuthamini huduma inayotolewa na watoa huduma binafsi za mifugo vijijini ili kutoa hamasa kwa watoa huduma hizo na kufanya kazi zao kwa ufanisi na umakini zaidi.
Wito huo umetolewa na Afisa Mdhamini Wizara ya kilimo na Mifugo Pemba Dr. Suleiman Mohamed Shehe huko Vitongoji wakati alipokuwa akichangia mada katika mkutano wa siku moja wa kutathmini utekelezaji wa program za kuimarisha kilimo na mifugo.
Alisema watoa huduma hao wanamchango mkubwa kwa jamii kwani kuna uhaba wa watoa huduma hizo vijijini hivyo ipo haja kwa jamii kuwapa ushirikiano ipasavyo ili kuendeleza huduma zao hizo.
Ameongeza kuwa Serikali imeamua kuwapatia elimu watoa huduma hao kwa lengo la kupunguza uhaba uliopo kwa sasa na uwepo wa watoa huduma hao kunapelekea kutatua matatizo yaliyopo katika jamii hususani vijijini.
Aidha alisema Wizara ya kilimo kupitia program ya kuwaendeleza wakulima na wafugaji itaendelea kutoa elimu kwa wanajamii ili kuongeza idadi ya watoa huduma hizo ili kupunguza mzigo kwa serikali.
Kwa upande wao watoa huduma hao wamesema kwa sasa idadi ya watoa huduma binafsi vijijini imeongezeka kutoka watoa huduma 40 hadi 56 ambapo kati yao 9 ni wanawake na 47 na wanaume.
Aidha wameongeza kuwa elimu waliyopatiwa kupitia program ya kuwaendeleza wakulima na wafugaji imewajengea uwezo wa kitaalamu na kuweza kupunguza matatizo yanayowakabili wafugaji na kuongeza wigo wa utoaji huduma za msingi vijijini.
Walisema kuwa wamekuwa msingi wa kutoa huduma kwa wafugaji vijijini katika mambo ya tiba na ushauri chini ya usimamizi wa wataalamu wa idara ya mifugo na kwa sasa wameanza kuaminiwa na wafugaji.
Pia walisema huduma wanazotoa huzingatia zaidi misingi ya kusaidiana kwani ni nafuu ukilinganisha na wafanya biashara kwani na wao ni wafugaji.
Watoa huduma hao wameiyomba wizara ya mifugo kuwaombea fursa zaidi ya kujiendeleza kielimu katika chuo cha kilimo kizimbani ili kuendeleza elimu waliyoipata na kuendeleza ufanisi zaidi wa kazi zao za kila siku kwani wao kutohuduma wanachukulia kama ni ajira.
“Baada ya kujengewa uwezo tumeweza kujitegemea kwa mambo madogo madogo na huduma hizi zimeanza kuwa ni chanzo cha mapato kwa familia zetu hivyo tunaomba serikali kutuombea nafasi katika chuo cha kilimo kizimbani ili kujiendeleza kielimu zaidi”,Walisema wakulima hao.
Wakizitaja changamoto wanazokabiliana nazo katika utoaji wa huduma hizo walisema ni pamoja na tatizo la usafiri kwani hutembea masafa marefu kuto huduma hizo,upungufu wa vitendea kazi pamoja na uhaba wa elimu hasa katika huduma ya mambo ya upandishaji kwa shindano(A.I)

No comments:

Post a Comment