Wakati wa shambulio la tarehe 24 Aprili, washambuliaji walimpiga kwa rungu na kumvunja mkono meneja Mohamed Ahmed Jama, ambaye anajulikana kama Aloley. Washambuliaji walidaiwa pia kujaribu kumpiga risasi lakini walishindwa. Mmoja wa washukiwa alikimbia, wakati mwingine alikamatwa na kujulikana kuwa ni ofisa wa polisi.
"Mtu anayetuhumiwa hatasamehewa kwa kuwa ni sehemu ya polisi," aliapa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Mkoa wa Somaliland Mohamed Nur Arrale ambaye alisimama mbele ya bunge la mkoa huo kwa ajili ya kuhojiwa tarehe 29 Aprili. Alilaani shambulio hilo, akiitaja kitendo hicho kuwa cha ukatili ambacho ni kinyume na kile ambacho serikali ya mkoa wa Somaliland na watu wake wanasimamia.
Waziri huyo pia alitahadharisha juu ya kuunganishwa kwa ofisa wa serikali kwenye shambulio hilo au kuruka kabla ya uchunguzi.
Mkuu wa polisi Brigedia Jenerali Abdullahi Fadal Iman, ambaye pia alisimama mbele ya bunge kuhojiwa, aliwaambia wabunge kwamba uchunguzi wa suala hilo unaendelea.
Huku polisi bado wanaendelea kumtafuta mshukiwa aliyeponyoka, askari polisi aliye chini ya ulinzi atafikishwa mahakamani hivi karibuni, Iman alisema.
Hata hivyo, Aloley, ambaye alisema anaendelea vizuri kupata nafuu kutokana na shambulio hilo, alielezea kutoridhika kwake na namna polisi wanavyoshughulikia suala hilo hadi sasa na akatoa wito wa uchunguzi huru.
"Nina imani kwamba tulishambuliwa kwa sababu ya kazi yetu ya uandishi wa habari na maandiko tunayosambaza kwa umma," aliiambia Sabahi.
Hivi karibuni, Hubaal iliweka wazi masuala kama vile rushwa na taratibu zisizo za kawaida za ununuzi unaofanywa na maofisa katika utawala wa mkoa, na utata juu ya uchimbaji wa mafuta huko Somaliland.
"Tuna ushahidi wa kuunganisha maofisa wa serikali [na washambuliaji]," alisema. Kwa mujibu wa Aloleiy, simu ya mkononi iliyookotwa na wafanyakazi wa Hubaal baada ya shambulio ilionyesha mawasilaino kamili baina ya mshambuliaji aliyekamatwa na ofisa wa serikali. Simu hiyo ilipewa polisi baada ya kuwasili katika eneo la tukio.
Wito wa uchunguzi huru
Mashirika ya haki za binadamu, waandishi wa habari na viongozi wa vyama vya upinzani waliunga mkono wito wa Aloley kuhusu uchunguzi huru."Kwa kuwa watu waliojaribu kufanya mauaji ni pamoja na ofisa polisi, uchunguzi unapaswa kufanywa na tume huru," alisema Ahmed Yusuf Hussein, mkurugenzi wa Horn Human Rights Umbrella. "[Kutokana na mgongano wa kimaslahi katika kesi hii], polisi hawawezi kuaminika kusimamia uchunguzi, maombi yetu ni uchunguzi kufanywa na kundi huru."
Ili kupata matokeo yatakayokubalika, serikali ya mkoa lazima ifanye upelelezi wa kesi hii kwa haki, alisema Mohamed Abdi Urad, makamu mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Somaliland.
"Tunaamini kwamba, kwa kiasi kidogo sana kikundi huru kitakuwa sehemu ya uchunguzi kwa kuwa washukiwa ni wafanyakazi wa serikali," Urad aliiambia Sabahi.
"Kama [wakosaji] hawatawajibishwa kwa haki, inaweza kusababisha machafuko katika nchi kwa sababu jamii yetu ina utamaduni wa kulipiza kisasi," alisema, akiongeza kwamba kama waandishi wa habari wataogopa kufanya kazi yao, hali hiyo itadhoofisha uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari vilivyo huru.
"Na madhara ya hali hiyo yatakuwa ni kupotosha ukweli," alisema.
Wabunge washindwa kuunda tume huru
Wakati huo huo, kamati ndogo ya mambo ya ndani, ulinzi na usalama ya bunge la Somaliland imetoa wito katika huduma za usalama wa mkoa kuwapeleka wahalifu na wasaidizi wao mahakamani. Vyama viwili vya upinzani, Chama cha Haki na Ustawi (UCID) na Wadani, viliungana na kulaani shambulio na kutoa wito huo huo wa kuunda uchunguzi huru."Hakukuwa na mgogoro kati ya watu waliofanya shambulio na gazeti hilo, kwa hiyo, ni wazi kwamba serikali iliwatumia watu wenye silaha [kufanya shambulio hilo]," alisema Hassan Essa Jama, mwanasiasa na makamu wa raisi wa zamani wa Somaliland.
Katika tamko lililotolewa tarehe 27 Aprili, makamu wa rais wa zamani wa mkoa alitoa wito kwa wabunge wote wa Somaliland kuunda tume huru kuchunguza kesi hiyo.
"[Shambulio] hilo ni hatua ya kuona makosa mabaya zaidi, mauaji, udhalilishaji na bugudha miongoni mwa umma," alisema.
Pamoja na wito kadhaa wa kuunda tume huru, hadi sasa hakuna tume iliyoundwa.
Katika maeneo mengine ya Somalia, waandishi wa habari wanne waliuawa huko Mogadishu mwaka huu, wakati waandishi wa habari wengine 18 wa Somalia waliuawa mwaka 2012 nchini.
No comments:
Post a Comment