Licha ya kupita miaka 40 tangu Uingereza ijiunge na Muungano wa Ulaya
( wakati huo jina lilikuwa Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya), bado mabishano
yangaliko miongoni mwa raia wa visiwa hivyo kuhusu „kero“ ndani ya
Muungano huo, na kama ni bora hivi sasa nchi hiyo ijitoe. Hali hiyo
imezifanya nchi nyingine shirika ndani ya Muungano huo kulalamika kwamba
Uingereza ni korofi, inazuwia mwenendo wa kuzidi kuiunganisha Ulaya
itakayokuwa imara zaidi na huenda siku moja kuwa na serikali moja.
Licha ya kwamba Januari mwaka huu waziri mkuu wa Uingereza, David
Cameron, alitangaza kwamba huenda, baada ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka
2015, na pindi yeye atashinda katika uchaguzi huo, Waingereza wakatakiwa
wapige kura ya maoni hapo mwaka 2017 kama wanataka nchi yao ibakie
ndani ya Muungano wa Ulaya, bado kuna wabunge kutoka chama chake
mwenyewe cha Conservative walioonesha hawajatosheka tu na ahadi hiyo ya
kiongozi wao. Walitaka zaidi, na kumbinya Cameron aweke wazi- kupitia
sheria itakayotungwa- kwamba kura hiyo ya maoni hakika itafanyika, na
isitegmee chama chake kushinda uchaguzi ujao au yeye kubakia madarakani
hadi wakati huo. Pia wala isitegemee matokeo ya mashauriano ambayo
Uingereza inataka yafanyike ili ijipatie masharti mepya yalio bora
kuweza kubakia katika Muungano huo.
Wiki iliopita wabunge 130, wengi wao wakiwa kutoka Chama cha
Conservative ambao wanakerwa na mfumo wa Muungano wa Ulaya na namna nchi
yao inavotendwa, waliwasilisha bungeni mswada uliolaumu msimamo wa
serikali yao kuelekea Muungano huo. Ilikuwa kama kumpiga kibao cha usoni
David Cameron. Mswada huo ulishindwa kupita bungeni, lakini ulitoa
ishara muhimu ya kisiasa.
Ni wazi kwamba hisia za Waingereza wengi kupinga nchi yao kubakia
ndani ya Muungano wa Ulaya zinazidi, japokuwa wachache kati yao ni
kutokana na uzalendo kuliko kuangalia hali halisi ya mambo. Mada juu ya
werevu wa kuitisha kura ya maoni inabakia katika vichwa vya habari, na
hata katika chaguzi za karibuni za serikali za mitaa chama cha Ukip,
kinachotaka Uingereza itoke kutoka Muungano wa Ulaya, kilifanikiwa
kupata kura nyingi za kutoka wanachama wa chama tawala cha Conservative.
Chama hicho cha Ukip katika uchaguzi ujao huenda kikaweza kukipotezea
ushindi chama cha Conservative, na kuwacha njia wazi kwa chama cha
Labour kuingia madarakani. Wanachama wengi wa Chama cha Conservative
hivi sasa wanataka viongozi wao watamke wazi na bayana kuhusu nchi yao
kubakia ndani ya Muungano.
Kilichowaudhi wabunge hao waliowasilisha mswada wao ni kwamba katika
hotuba ya karibuni alioitoa malkia bungeni- ambayo ni programu ya
serikali kwa siku zijazo- hakujatajwa kwamba serikali itawasilisha
rasimu ya sheria bungeni kuhusu kuitishwa kura ya maoni. Kwa hakika
David Cameron asingepinga serikali yake kuwasilisha rasimu ya aina hiyo.
Lakini ana tatizo. Nalo ni kwamba serikali yake ni ya mseto ambapo
ndani yake kuna chama cha Liberal Democratic kinachopinga au mara
nyingine kutia na kutoa kuhusu suala la kuitishwa kura ya maoni. Kwa
hivyo, Cameron alijitafutia njia ya katikati, kuihifadhi nafasi na
heshima yake ya kisiasa katika chama chake na, wakati huo, angalau,
kuwaridhisha wabunge wa chama chake. Aliwakubalia kichinichini wabunge
hao wawasilishe mswada wao, akijuwa wazi kwamba hautapita, kwani
utapingwa na kura nyingi za wabunge wengine wa chama chake cha
Conservative, wale wa chama kikuu cha upinzani cha Labour na pia wa
chama cha Liberal Democratic. Na hilo ndilo lilotokea.
Kama yalivyo mabishano miongoni mwa raia, hali ni vivyohivyo ndani ya
vyama vikuu vya kisiasa huko Uingereza. Chama kikuu cha upinzani cha
Labour, licha ya kufurahia mabishano yaliozuka ndani ya chama cha
Conservative, nacho kina wasiwasi na wazo la kuitishwa kura ya maoni,
kikihofia hali itakayochomoza pindi wananchi wengi wataipa mgongo Ulaya.
Chama hicho kinaiona taswira ya Uingereza itakayozidi kutengwa na
Ulaya. Na japokuwa matokeo ya kura ya maoni yatabidi yaheshimiwe kwa
vyovyote, lakini hakitaki kubeba dhamana wa mustakbali usiojulikana.
Chama cha Labour kinapendelea Uingereza ifanye mashauriano zaidi hivi
sasa na izidi kuzibinya nchi nyingine za Muungano huo ziyaridhie matakwa
yake na kuziondoa zile inazoziita „kero“ za Muungano. Baadhi ya
viongozi wa Chama cha Labour wameweka wazi kwamba pindi patakuweko
mabadiliko ya mkataba wa sasa wa Muungano ambayo yatabadilisha wizani wa
nguvu, ambapo matakwa ya Uingereza yatakubalika, basi huenda wao
wataunga mkono iitishwe kura hiyo ya maoni. Na suala muhimu ni kama kura
hiyo ya maoni itakuwa ni kujibu suali moja tu- nalo: Uingereza ibakie
ndani ya Muungano wa Ulaya au itoke?
Waingereza kadhaa wanaziona faida za Muungano wa Ulaya kama taasisi
yenye kuendeleza utandawazi na uchumi wa kiliberali ndani ya soko la
watu milioni 500. Lakini wana wasiwasi juu ya mipango ya Muungano huo ya
kuziwekea kanuni kali taasisi za fedha na mabenki ambayo mengi
yanafanya shughuli zao mjini London, hivyo mji huo kuwa kituo muhimu cha
shughuli za fedha duniani. Pia chama cha Conservative hakiridhishwi na
sheria za ajira za Muungano huo, hasa zile zinazohusu masaa ya kufanya
kazi, ambazo inaona zinazibana shughuli za kibiashara za Uingereza.
Malalamiko yamezagaa huko Uingereza kwamba Uingereza huwekwa pembeni
yanapokuja masuala muhimu ya siasa ya fedha, kwamba Tume ya Umoja wa
Ulaya huko Brussels hujititimua na kuonesha misuli kama vile ni serikali
ya Ulaya, inajiingiza katika mambo ambayo ni dhamana za serikali za
nchi wanachama, licha ya kuwa pia na bajeti kubwa inayopita kiasi.
Licha ya kwamba asilimia 70 ya watu wa visiwa hivyo wanataka iitishwe
kura ya maoni kuhusu mustakbali wa nchi yao ndani ya Ulaya, wako baadhi
yao wanaotambua kwamba kuna mambo mengi ya kuwashughulisha zaidi-
madeni ya serikali yanayozidi, uchumi kukwama na kashfa za kisiasa
zisizokwisha. Pia wanakumbusha kwamba nusu ya uekezaji wa moja kwa moja
nchini humo unatokea nchi nyingine za Muungano wa Ulaya, na nusu ya
bidhaa ambazo London inasafirisha ng’ambo zinakwenda katika nchi za
Muungano. Wanadai kwamba kujitoa kutapunguza nafasi za ajira, kutafanya
uhusiano wa kimataifa wa nchi yao unywee na kutapunguza utajiri wa nchi
yao.
Manung’uniko hayo ya Uingereza yanawakumbusha watu wa Ulaya juu ya
shakashaka alizokuwa nazo rais wa Ufaransa, marehemu Charles de Gaulle,
pale Uingereza ilipoomba kuwa mwanachama wa Muungano wa Jumuiya ya
Kiuchumi ya Ulaya. Yeye aliashiria kwamba Waingereza, kama wanavisiwa,
wana hamu kubwa ya kulinda uhuru na heshima ya utawala wao.
Kinachoonekana sasa ni kwamba kwa Waingereza kwao Muungano wa Ulaya ni
njia tu ya kufikia lengo walilokusudia na si kwamba Muungano huo ni
makusudio na lengo lao la mwisho.
Kuna nchi ndani ya Muungano ambazo haziko tayari kuikubalia Uingereza
kile inachotaka. Zinahoji kwamba nchi hiyo iliingia ndani ya klabu na
ikakubaliana na mashrati ya klabu hiyo pale ilipojiunga, hivyo si haki
kutaka kanuni za klabu kutoka sasa zipindwe ili kuiridhisha.
Haiwezekani, na kama haitaki basi ina hiyari ya kujitoa. Na yaonesha
Waingereza nao huenda wakaamua kutafuta njia mbadala.
Kwa baadhi ya wachunguzi wa mambo ni kwamba Waingereza wanautaka
Muungano wa Ulaya, lakini kwa bei wanaojiwekea wenyewe, na sio kwa bei
inayokubaliwa na wanachama wengine. Waingereza wanausahau ule usemi wao
wenyewe kwamba mtu hawezi kubakia na keki yake huku anaila. Pia, lakini,
wananchi wana kila haki ya kutaka wapige kura ya maoni, licha ya kile
kitisho cha msemo wa Kiswahili: Mtoto akililia wembe mpe.
Othman Miraji Othman
Cologne/Ujerumani
Nambari ya simu: 0653-466577 au +49-2233-21721
e-mail: mwinjuu@hotmail.com
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment