Monday, June 3, 2013
SMZ: Muungano ukivunjika Tanganyika na Zanzibar zitayumba
Akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo Chambani huko Pemba, Balozi Seif alisema wako wanasiasa wanaopigania maslahi binafsi wakiwa na lengo na kuisambaratisha misingi ya Mapinduzi na Muungano.
Alisema Tume ya mabadiliko ya Katiba haikuundwa kwa malengo ya kuvunja muungano na kuwataka wananchi kujiepusha pia wakitafakari kwa umakini na utulivu kwa vile athari za kuvunjika kwa muungano ni kubwa kuliko inavyotazamiwa.
“Tume ya mabadiliko ya katiba haina hadidu ya rejea ya kuvunja muungano, wanachotakiwa wazanzibari kuainisha kasoro zote zilizopo na kuzipatia ufumbuzi bila ya kuongozwa na jazba ya kuvunja muungano uliopo,”alisema Balozi Seif.
Akionekana kushagazwa na matamshi ya baadhi ya wanasiasa wanaotaka muungano wa mkataba bila ya kuonyesha mfumo wa uendeshaji wake, alisema iwe ni mwiko kwa watu hao kutumia jina la wazanzibari wote kwamba hawataki muungano uliopo.
Alisema kuna kikundi cha watu ambao mawazo yao kwa miaka mingi ni kuukataa muungano na si Wazanzibari wote huku akisema kwamba muungano huo umeleta tija na faida zaidi kwa Wazanzibari kuliko Watanganyika.
“Wenye maduka makubwa, wafanyabiashara, wakulima na majumba ya kifakhari huko Tanzania Bara ni Wazanzibari tena wenye asili ya Pemba, kuvunjika kwa muungano kutawapa athari na hasara badala ya faida zinazopatikana sasa,”aliasa Balozi Seif.
Alisema maneno hayo ya kishabiki ni sawa na kuwakaangia mbuyu watu waliojijenga kiuchumi, kimiradi na kimaendeleo kwasababu alisema anaamini nje ya muungano lolote lenye hasara na mtikisiko linaweza kutokea.
“Amani na umoja wa kitaifa ukivurugika, kina mama na watoto ndiyo waathirika wakubwa, amani ni mfano wa mke ukimpa talaka ni taabu kumpata tena, tumezishudia nchi za Sudan Kusini na Kaskazini, Ethiopia na Eritrea, zimeyumba na kukosa utulivu wa ndani,”alisema.
Aidha alisema inashangaza kusikia baadhi ya watu hasa wanasiasa wakisema Wazanzibari wote hawataki muungano bila ya kutoa takwimu na ushahidi wa maneno hayo, walikutana wapi, waliazimia mambo gani kuhusu jambo hilo hadi kujumuishwa na kudaiwa hawataki muungano.
Msimamo huo wa Serikali umekuja kufuatia kongomano lililokuwa likijadili mwelekeo wa Muungano wakati huu wa mjadala wa katiba mpya ambalo lilifunguliwa na Makamo wa kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad katika ukumbi wa Bwawani mjini Zanzibar mwishoni mwa wiki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment