Tuesday, December 25, 2012

Kenya yaanzisha uchunguzi kuhusu milipuko ya Eastleigh

Na Rajab Ramah, Nairobi

Desemba 24, 2012
Mfululizo wa mashambulizi ya mabomu na makombora ya hivi karibuni katika kitongoji cha Nairobi cha Eastleigh umefanya wakazi wawe katika hofu na maafisa kuwa na wasiwasi juu ya matendo yanayoendelea ya vurugu yanayokusudiwa kuchochea migongano ya kikabila na kidini nchini Kenya.

  • Maafisa polisi wa Kenya wakilinda eneo lilipotokea shabulio la makombora matatu tarehe 16 Disemba lililolenga baa katika kitongoji cha Eastleigh mjini Nairobi. [Na Tony Karumba/AFP]
  • Afisa polisi wa Kenya akizungumza na wapangaji wa nyumba jirani wakati wa msako wa nyumba kwa nyumba kufuatia shambulio la kombora la tarehe 16 Disemba huko Eastleigh. [Na Tony Karumba/AFP]
Mashambulizi ya hivi karibuni yalianza mwezi Novemba na kuendelea mwezi mzima uliopita. Hapo tarehe 18 Novemba, watu wanane waliuliwa na dazeni kujeruhiwa katika mlipuko wa basi dogo uliotokea huko Eastleigh. Shambulio hilo lilizuamapambano ya baina ya makabila kwa muda wa siku mbili ambayo yalipelekea kujeruhiwa kwa watu 10 na kuharibiwa kwa mali nyingi.
Hapo tarehe 5 Disemba, bomu la kutegwa kando ya barabara liliua mtu mmoja na kuwajeruhi wanane wengine huko Eastleigh. Siku mbili baadaye,guruneti lilivurumishwa katika kundi la waumini waliokua wakitoka katika msikiti maarufu wa Hidaya. Mlipuko huo uliua watano na kujeruhi wengine 16, akiwemo mbunge na mlinzi wake.
Serikali ilianzisha msako wa usalama kufuatia milipuko hiyo, na kuwatia mbaroni washukiwa 600, wengi wao wakiwa wahamiaji haramu wanaoishi nje ya makambi ya wakimbizi ya Dadaab, kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo.
Lakini milipuko imeendelea kuitikisa Eastleigh. Siku ya tarehe 16 Disemba, watu wawili walijeruhiwa vibaya sana wakati kiasi chamakombora matatu yalilengwa katika baa karibu na msikiti wa Hidaya. Polisi waliwakamata washukiwa tisa kuhusiana na shambulio hilo.
Siku mbili baadaye, milipuko miwili iliwajeruhi kiasi cha watu wawili karibu na msikiti kwenye eneo la Panganihuko Eastleigh. Polisi aliwakamata watu 23 baada ya milipuko hiyo na kuwasaili ili kujua kama wana habari zozote muhimu juu ya mashambulizi hayo, kwa mujibu wa Mkuu wa polisi wa Nairobi Moses Nyakwama.
Hakuna kikundi kilichodai kuhusika na mfululizo wa mashambulizi haya, lakini maafisa kwa kiasi kikubwa wanawalaumu wanamgambo wa al-Shabaab, wenye uhusiano na al-Qaida, ambao wameapa kutekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi nchini Kenya ili kupinga uwepo wa Jeshi la Ulinzi la Kenya nchini Somalia.

Serikali ya Kenya yaanzisha tume ya uchunguzi

Ili kufikia kwenye kiini cha mashambulizi ya karibuni ya kigaidi na kutafuta suluhisho, serikali itaunda tume ya uchunguzi ya watu kumi, yenye maafisa wa serikali watano na wajumbe watano watakaopatikana kutoka jamii ya wafanyabiashara wa Eastleigh.
Uamuzi wa kuundwa kwa tume hiyo ulikuja Alhamisi (tarehe 20 Disemba) baada ya Waziri Mkuu Raila Odinga kuongoza mkutano na Waziri wa Uhamiaji Otieno Kajwang, Waziri wa Maendeleo kwa Kaskazini ya Kenya na Maeneo Mengine yenye Ardhi Kame Mohammed Elmi, Mkurugenzi Mkuu wa Kikosi cha Intelijensia ya Usalama wa Taifa Michael Gichangi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Mutea Iringo na wafanyabiashara wa Eastleigh.
Wajumbe wa tume hiyo bado hawajatajwa, lakini polisi, Idara ya Intelijensia ya Usalama wa Taifa, Waziri wa Maendeleo ya kaskazini mwa Kenya na Ardhi Nyingine Kame, Wizara ya Uhamiaji na ofisi ya waziri mkuu, kila moja itachagua mjumbe moja. Kwa kuongezea, wawakilishi wa wafanyabiashara watateuliwa na mwenyekiti wa Chama cha Wilaya ya Biashara Eastleigh Hassan Guled.
Tume hiyo ambayo itaongozwa na Iringo, itapaswa kuanza kazi mara moja, ofisi ya waziri mkuu ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Odinga alielezea wasiwasi wake kwamba mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi huko Eastleigh yanaharibu sura ya Kenya na yanaangamiza sekta ya utalii. Aliipa kazi timu hiyo ya kutafuta sababu za mashambulizi hayo na kutatua tatizo papo hapo ili kushughulikia hali hiyo.
Waziri mkuu aliwaomba wananchi kushirikiana na tume ya uchunguzi kwa kutoa habari muhimu zitakazosaidia kuwasafisha magaidi na wafuasi wao.
"Ninaitaka jumuiya ya wafanyabiashara katika Eastleigh na wenyeji vilevile, kujitolea kwa kutoa habari yoyote ambayo itawezesha kuwakamata wahalifu hawa na kuwapeleka mbele [ya sheria]," Odinga alisema katika taarifa.
Alilaani kuinyooshea vidole kikabila jamii ya Wasomali na kusema kuwa hiyo imepelekea mashambulizi ya kikabila dhidi ya watu wasio na hatia na lazima hilo lisitishwe. "Kisilaumiwe kikundi chochote cha kikabila kwa makosa yaliyofanywa na mtu mmoja miongoni mwao," Odinga alisema.
"Kama sehemu ya suluhisho kwa mashambulizi haya ya kigaidi, tunataka kuendesha elimu ya uraia katika maeneo yaliyoathiriwa ili kuwahamasisha watu dhidi ya kujihusisha na shuguli za kigaidi au kuwaunga mkono wahalifu," alisema wakati wa mkutano katika ofisi yake siku ya Alhamisi.

Jamii ya Eastleigh yajibu

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wilaya ya Biashara Hassan Guled aliiambia Sabahi kuwa anakaribisha hatua ya serikali kwa vile ukuaji wa hali ya kutokuwepo kwa amani sio tu imechukua maisha ya watu, bali imeharibu biashara pia.
Alisema kuwa mashambulizi ya maguruneti yalikuwa yanaangamiza mahusiano baina ya Wakenya wenye asili ya Somalia na jamii nyingine zinazoishi katika eneo hilo.
"Kile kinachokuwa kinaendelea hapa Eastleigh ni aina fulani ya kupambana na moto [baina ya wahalifu na jamii] ambapo kila mtu [kwa kutumia vurugu] baada ya shambuio la kombora ... lakini ni matumaini yetu kuwa timu hii itasaidia [kufichua] nyuso zilizoko nyuma ya mashambulizi haya na kuzuia matendo ya kihalifu yasitendeke kwa muda mrefu," alisema.
Guled aliwataka wananchi kushirikiana na timu ya uchunguzi na kuwaomba polisi wasiwaachie huru washukiwa wa kigaidi ambao wamekamatwa, kwa kusema kuwa tendo kama hilo litarudisha nyuma juhudi za kudumisha usalama.
Wakati huo huo, wakazi wa Eastleigh walipokea tangazo kuhusu tume mpya kwa hisia mchanganyiko.
Said Ali, mwenye umri wa miaka 30 na muuza duka katika Garissa Lodge huko Eastleigh, alisema kuwa alikuwa na matumaini kuwa mkabala huo mpya wa serikali utasaidia kuzuia mashambulizi, pamoja na kuzuia polisi wasiitenge jamii ya Somalia.
"Ingawaje kumekuwepo [na jamii] iliyopigwa sana na mashambulizi haya, serikali daima imekuwa ikijibu maeneo yaliyotokea milipuko hapa kwa kutoa adhabu ya kuwahusisha wote na kila mmoja [mwenye mahusiano na Somalia] analaanwa na kufanywa mhalifu, alisema. "Tunaitwa al-Shabaab kwa sababu tu tumezaliwa Somalia. Tunatumai kuwa timu ya uchunguzi sio itabadlisha picha ya hapa bali pia kuhakikisha usalama wetu."
Abdirizak Abdi, mwenye umri wa miaka 60, mzee wa Eastleigh, aliiambia Sabahi kuwa jamii iko tayari kuisaidia timu ya uchunguzi, lakini akasema kuwa serikali kwanza inapaswa kuwaelemisha watu juu ya umuhimu wa kushirikiana na mashirika ya usalama.
Watu wengi wa eneo hilo wataachana na mchakato huo ikiwa serikali itashindwa kuwahakikishia kuwa hawatakuwa wahanga wakati watakapojitolea kutoa taarifa, alisema, na kuongeza kuwa watu walikataa kusaidia uchunguzi kwa sababu polisi walikuwa wanamshughulikia kila Msomali kama mshukiwa.
"Watu wanapaswa kuelemishwa juu ya kwa nini wanahitaji kushirikiana na kuhakikishiwa usalama wao," Abdi alisema.

No comments:

Post a Comment