Katika ujumbe wa sauti uliotolewa mwezi wa Disemba na al-Kataib Media Foundation, tawi la habari la al-Shabaab, kiongozi wa al-Shabaab Ahmed Abdi Godane, anayejulikana pia kama Mukhtar Abu al-Zubair, alikubali kadamnasi kuwa wapiganaji wa al-Shabaab walikuwa wameshindwa katika mfululizo wa vita dhidi ya vikosi vya Somalia na washirika wake. Katika ujumbe huo, aliwataka watu wa Somalia kusimama imara na kukisaidia kikundi chao kifedha.
"Ninapenda kuwaambia Waislamu wa Somalia kusimama imara kwa ndugu zenu waaminifu wa mujahidina na muwape fedha kwa vile wanapigana kuulinda Uislamu," alisema.
Ali Mohamed Hassan, mwakilishi wa zamani wa al-Shabaab huko mkoa wa Banadir, aliwataka wakaazi na wafanyabiashara wa Mogadishu hapo tarehe 25 Disemba watoe msaada wa kifedha kwa al-Shabaab ili iweze kugharamia operesheni zao za kijeshi. "Tunawataka wafanyabiashara wawasaidie mujahidina na watoe fedha zao kwa jina la Mwenyezi Mungu," alisema.
Hata katika ya miezi ya kabla ya Juni, kabla ya kikundi kuipoteza kimkakati Kismayu, Godane aliyataka makabila ya Somalia kuunga mkono kikundi cha wanamgambo dhidi ya serikali ya Somalia. Chini ya wiki moja baadaye,Yusuf Sheikh Isse, kiongozi wa al-Shabaab katika mkoa wa Shabelle ya Kati, aliyatolea wito makabila na wafanyabiashara kufanya michango ya kifedha kwa ajili ya operesheni za kikundi.
Mazingira magumu ya kifedha
"Kikundi hicho chenye msimamo mkali cha al-Shabaab kwa sasa kinapitia katika hali ngumu kabisa kifedha hali ambao hawaijapata kwa miaka, na miito yao mfululizo ya kuyataka makabila na wafanyabiashara wa Somalia kutoa michango ya fedha kunaakisi mgogoro wa kifedha ambao unakikabili," alisema Omar Farah, mhariri wa Kiarabu wa Shirika la Habari la Taifa la Somalia."Pia hawawezi kugharamia operesheni zao za kigaidi kutokana na matatizo ya kifedha yanayowakabili, jambo ambalo limesababaisha udhaifu na kuporomoka kwa kikundi hicho," aliiambia Sabahi.
Katika mahojiano na gazeti la al-Hayat la London hapo tarehe 29 Disemba, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema kuanguka kwa al-Shabaab kuko karibu. "Al-Shabaab imeanza kuanguka na kusambaratika," Mohamud alisema. "Uongozi wao mkuu umeshindwa na wapiganaji wake wameanza kukimbia."
"Al-Shabaab kwa sasa wako dhaifu kijeshi na wanaweza kushindwa karibuni, lakini tatizo ni kung'oa itikadi yao ya msimamo mkali mara [wapiganaji hao] watakapoingizwa tena katika jamii," alisema.
Jaribio la mwisho la kikundi hicho la kukusanya michango liko katika kupata msaada wa makabila kuliko itikadi yao, ambayo hatimaye nayo inaonesha matatizo makubwa ya kifedha ambayo al-Shabaab inawakabili na kuchanganyikiwa kwao, alisema mchambuzi wa masuala ya kisiasa Mohamud Yusuf.
"Al-Shabaab imepoteza vyanzo vyake vya fedha tangu pale wanachama wake walipotimuliwa kutoka Mogadishu, Kismayu na vituo vyengine vya biashara, ambayo vingewapatia mapato makubwa kupitia kodi," Yusuf aliiambia Sabahi. "Kwa sababu hii, kikundi kinajaribu kwa kukata tamaa kuyalazimisha baadhi ya makabila na wafanyabiashara katika juhudi zake za operesheni za kijeshi."
Wafanyabiashara wakataa ombi la al-Shabaab
Hassan Mohamed, mfanyabiashara mjini Mogadishu, alisema kuwa wito wa al-Shabaab kwa wafanyabiashara kugharamia operesheni zao za ugaidi zitakuwa za bure tu."Wafanyabiashara wa Somalia wamekuwa wakichoshwa na ujanja wa al-Shabaab kwa vile kikundi kingeweza kuchukua fedha zao kwa nguvu chini ya kisingizio cha zaka au kwa jina la jihadi ya uongo," Mohamed aliiambia Sabahi. "Kumzamisha mtu na baadaye kumtaka mtu huyo huyo akupe msaada huku akizama huwa haina mantiki. Wito wa al-Shabaab kwa wafanyabiashara kuwa wawasaidie hauna tofauti sana na hilo."
Mukhtar Sheikh Abdullahi, muuzaji chakula wa jumla katika soko la Bakara, alisema wafanyabiashara wa Somalia wanakataa wito wa al-Shabaab wa kutaka wasaidiwe.
"Je, Al-Shabaab itajenga shule, chuo kikuu au nyumba ya kulelea mayatima ili wawaombe wafanyabiaashara wachangie fedha zao? Jawabu kwa swali hili kiufupi ni hapana," aliiambia Sabahi. "Kwa sababu hii, si haki kwa wafanyabiashara kutoa fedha zao kwa magaidi wanaowaua wananchi wasio na hatia."
"Tunapenda kuwaambia al-Shabaab na wanachama wake wakae kando na watuache peke yetu tuishi maisha tutakayotaka kuyachagua kuishi. Tunataka tuwe huru kuweza kufanya biashara," alisema.
No comments:
Post a Comment