Mogadishu inashuhudia wimbi la mizozo ya umiliki wa ardhi kutokana na kurejea kwa maelfu ya Wasomali kutoka ughaibuni.
Halimu wa Mahakama ya Wilaya katika eneo la Banadir Hashi Elmi Nur
alisema kuwa mahakama yake karibuni ilisajili kesi za migogoro ya ardhi
kwa kiwango kisichowahi kutokea. Alisema kuwa mahakama zinajaribu
kutatua kesi kama hizo haraka inavyowezekana kwa sababu migogoro hiyo
inaweza kuelekea kuwa mapigano.
"Kazi yetu inakatishwa na migogoro mingi miongoni mwa warithi wanao
kataa maelewano au kuja [katika Manispaa ya Mogadishu] kutatua migogoro
ya umiliki wa mali kwa sababu wamerithi ardhi hizo kutoka kwa familia
zao kulingana na mikataba ya kimila," Nur aliiambia Sabahi.
Alisema kuwa migogoro ya umiliki wa mali inakua kila siku kwa sababu
ilikuwa inashughulikiwa isivyo halali kwa miongo miwili iliyopita.
Nur pia alisema kuwa baadhi ya watu katika soko la Abdalla Shideye
mjini Mogadishu wanajinufaisha kutokana na nyaraka za kughushi za
umiliki wa ardhi, na kuongeza kuwa polisi watawakamata watu wanaohusika
na tabia hiyo na kuwafikisha mahakamani.
Watu mashuhuri wamenunua au kuchukuwa maelfu ya mita za mraba ya
ardhi kwa bei chee, jambo ambalo limesababisha migongano mikubwa ya
kikabila na kifamilia, alisema. "Sasa tunajaribu kurejesha nyumba na
mashamba ambayo yameuzwa au kuchukuliwa kwa nguvu kinyume cha sheria,"
alisema.
Meya wa Mogadishu Mohamed Ahmed Nur alionya dhidi ya ujenzi haramu wa
majengo na hoteli za kitalii katika maeneo karibu na ufukwe ambao wote
unamilikiwa na serikali ya Somalia.
"Kila mtu imuingie akilini kuwa ardhi yote iliyoko pwani kutoka
kaskazini hadi kusini ya nchi inamlikiwa na serikali ya shirikisho na
tunaweza kuona kwa macho yetu wenyewe vipi watu wanajaribu kuchukua
fursa ya hali tete ya utawala," alisema. "Wanajipa kiwango kikubwa cha
fedha kwa kuuza [zilizokuwa] makao makuu ya jeshi, kambi za kijeshi,
viwanja vya ndege vya kijeshi, hospitali na balozi. Tunapenda kutangaza
kuwa haya ni matendo haramu yanayofanywa na watu wasiokuwa wazalendo."
Kwa kuongezea, meya aliwataka wakaazi wa Mogadishu kuondoka katika
majengo ya watu binafsi ambayo wanayakalia visivyo halali na ardhi
nyengine za familia zilizokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe miongo
miwili iliyopita. Pia aliwataka watu waliokimbia makazi yao kuondoka
katika wizara, mashirika, hospitali na maeneo mengine yanayomilikiwa na
serikali jijini.
Nur alisema kuwa utawala wake utatuma ujumbe kwa mkuu wa kikosi cha
polisi kuwatia mbaroni wale wanaojaribu kudai ardhi inayomilikiwa na
Wizara ya Kazi za Umma na kuibadilisha kuwa mali binafsi au ya
uwekezaji.
Wakili Filsan Yusuf Siad alisema kuwa kukosekana kwa sheria na kanuni
kumesababisha utamaduni wa kupora na kuchukua ardhi za umma na za
binafsi.
Aliiambia Sabahi kuwa vikosi vya usalama vinapaswa kupambana na watu
mafisadi na watu maarufu wa makabila ambao wanajipa na kuuza ardhi
isivyokuwa halali.
"Nadhani kuwa ili kulitatua suala hili litakuwa gumu hadi pale polisi
itakaposimama pamoja na mahakama. Ikiwa sio hivyo, basi tutakuwa
mapinduzi ya umwagaji damu miongoni mwa wanaigombania," alisema.
Naye Mbunge Mohamed Mohamud Heyd alisema kuwa ardhi ya serikali
haipaswi kugeuzwa kuwa hoteli za kifahari au kutumiwa kwa madhumuni
mengine ya biashara.
"Nitalipeleka suala hili katika kikao cha bunge ili kufikia uamuzi
ambao utakomesha shughuli gharamu," Heyd aliiambia Sabahi. "Tunapaswa
tusiwe na huruma kwa suala haramu kama hilo ambalo linawafungulia
milango wazi wadanganyifu."
No comments:
Post a Comment