
Kwanza kabisa hatuna budi
kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na
kutuwezesha kukutana tena leo hapa hoteli ya Bwawani, ikiwa ni mara ya
kwanza kwangu kufanya mkutano kama huu kwa waandishi wa habari tokea
kuanza kwa mwaka huu mpya wa 2013. Naomba nichukue nafasi hii
kukutakieni kheri na Baraka tele katika mwaka huu wa 2013. Aidha, sina
budi kutoa shukurani zangu nyingi na za dhati kabisa kwenu nyote
waandishi mlioweza kuhudhuria hapa kwa wingi, licha ya kupewa taarifa
kwa muda mfupi, juu ya kuwepo kwa mkutano huu, lakini mkaukubali na
mkasema muje kusikiliza wito wetu.
Waheshimiwa waandishi wa habariKama ambavyo mnaelewa hivi sasa nchi yetu imo katika mchakato muhimu wa mabadiliko ya katiba. Mchakato huo ni jambo muhimu sana kwa sababu hii ni mara ya kwanza kabisa wananchi wa Tanzania wanashirikishwa kikamilifu katika kuamua aina ya katiba wanayoitaka, tokea katiba hiyo ilipotungwa mwaka 1977.
Tume ya mabadiliko ya Katiba katika kufanikisha kazi yake tayari imemaliza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, katika maeneo mbali mbali hapa Zanzibar na Tanzania Bara, na baada ya kumaliza hatua hiyo ya kukusanya maoni ya wananchi, tume hiyo ilianza kazi ya kukutana na makundi maalum, kwa ajili ya kuyasikiliza na kuchukua maoni ya makundi hayo, ambapo vyama tafauti vya siasa makundi mengine muhimu ya kijamii, zikiwemo taasisi za kidini yaliweza kupata fursa kama hiyo.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Baada ya tume hiyo ya mabadiliko ya Katiba kumaliza kuchukua maoni ya makundi maalum, jana tarehe 13 Januari, 2013 ilianza kukutana na viongozi mashuhuri kwa ajili ya kupata maoni.
Waheshimiwa waandishi wa habari
na furaha kukujuilisheni kuwa kwa mujubu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, mimi ndiye niliyepata bahati ya kuwa
wa kwanza katika kundi la viongozi mashuhuri kupewa nafasi ya kutoa
maoni yangu mbele ya Tume hiyo.
Baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji
Warioba na Makamu wake, Jaji Augostino Ramadhan jana asubuhi walifika
nyumbani kwangu Mbweni, kwa ajili ya kuja kunisikiliza kuchukua maoni
yangu kuhusu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo nimeona ni
jambo la busara wananchi nao wafahamu japo kwa uchache ni kitu gani
nilichokizungumza katika maoni yangu binafsi, kama Seif Sharif Hamad.Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama ilivyojitokeza kwa
Wazanzibari walio wengi, nami nimeona ni jambo la busara kabisa katika
maoni yangu nizungumzie moja kwa moja suala la Muungano wa Tanzania, kwa
vile nikiwa kama Mzanzibari niliwaeleza wajumbe wa Tume hiyo kuwa, hilo
ndilo jambo linalonigusa zaidi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Nukta muhimu nilizozizungumzia katika maoni yangu ni kama ifuatavyo:1. Asili na Sababu za Muungano
2. Misukosuko katika Muungano
3. Kiini cha matatizo katika Muungano
4. Uvunjwaji wa mkataba wa Muungano
5. Matatizo yatokanayo na kiini cha tatizo
6. Nafasi ya Zanzibar katika Muungano
7. Vipi tutoke hapa tulipo
8. Mfumo mpya wa Muungano wa Mkataba
ASILI NA SABABU ZA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Maoni yanayotolewa kuhusu asili
na sababu za Muungano yamekuwa yakitofautiana mno. Wapo wanaouleza
Muungano huu kuwa ni wa pekee katika bara la Afrika, kwani ndiyo pekee
ulioweza kudumu katika kutimiza azma na malengo ya kuleta umoja wa
Afrika (Pan-Africanism), na pia wapo wanauona kuwa ni “jaribio la
kusisimua la ukoloni mdogo wa nchi moja ya Kiafrika kuiteka na kuitawala
nchi nyengine ya Kiafrika”.
Hivyo basi, si rahisi kusema moja kwa moja kuwa maelezo yepi au hoja ipi ni sahihi. Utangulizi (Preamble)
wa Mkataba wa Muungano wa 1964 wenyewe unataja sababu kuu ya
kuunganisha nchi za Zanzibar na Tanganyika kuwa ni “maingiliano ya muda
mrefu ya watu wa nchi mbili hizi na mahusiano yao ya kidugu na kirafiki
na kuendeleza umoja wa watu wa Afrika. Lakini miaka 49 sasa baada ya
uzoefu wa Muungano huu, Wazanzibari wanajiuliza kweli haya yalikuwa
ndiyo madhumuni ya Muungano huu?
Tukiangalia kwa undani tutaona
kuwa wakati ule wa miaka ya 1950 na 1960 waasisi na wakuu wa harakati za
kupigania Uhuru waliiona mipaka ya nchi zao iliyowekwa na wakoloni kuwa
ni ‘mbinu za kibeberu’ zilizotekelezwa kwa ajili ya manufaa na maslahi
yao. Kutokana na hisia hizo, mazungumzo ya kuanzisha aina fulani ya
umoja miongoni mwa nchi huru za Afrika yalitawala duru za siasa.
Nadharia mbili zilijichomoza. Ya
kwanza, ikishadidiwa na Kwame Nkrumah wa Ghana, ilikuwa ikitaka
kuasisiwa kwa nchi moja tu ya Afrika nzima iliyoungana ikiwa na Serikali
moja kwa bara zima. Nadharia hii ilipingwa na baadhi ya viongozi,
wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika, ambao walisisitiza
haja ya kuanza na miungano ya maeneo (regional unions) chini ya mfumo wa
Shirikisho badala ya kuwa na mpango wa Serikali moja.[1]
Katika kulifikia lengo hilo, viongozi wa kisiasa wa nchi tatu za
Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanganyika – walikuwa wakifanya
mikutano ya mara kwa mara kipindi chote cha kati ya mwaka 1961 na 1963
kuona jinsi gani wanaweza kutimiza ndoto hiyo. Mfumo wa Muungano
uliokuwa ukiandaliwa ulikuwa ni ule wa Shirikisho.
Ijapokuwa Zanzibar
haikuwakilishwa katika mkutano wa kuanzishwa umoja wa Afrika Mashariki,
viongozi wan chi tatu hizo walisema kuwa “tunapaaswa kuweka bayana
kwamba nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika mikutano yetu
kwa ajili ya uundwaji wa Shirikisho.
Wakati juhudi za kuanzisha
Shirikisho la Afrika Mashariki zikiwa zinafifia, Mwalimu Nyerere aliona
Zanzibar kama fursa ambayo hakutaka kuipoteza. Katika mazungumzo ya siri
kati yake na Rais Abeid Amani Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,
wakakubaliana kuziunganisha nchi mbili hizi. Hakukuwa na ushirikishwaji
wa aina yoyote ule wa wananchi wa nchi hizi mbili katika maamuzi haya
makubwa. Usiri uliogubika hatua hii kubwa unafichuliwa na Mwalimu
Nyerere mwenyewe pale aliposema:
“Tanganyika tulipeleka Polisi
wetu Zanzibar. Baada ya kuyashinda matatizo kadhaa tukaungana. Sisi
wenyewe kwa khiyari zetu tulikubaliana kuungana. Karume na mimi
tulikutana. Peke yetu wawili tu tulikutana. Nilipomtajia wazo la
Muungano, Karume hakufikiri hata mara mbili. Pale pale alinitaka kuita
mkutano wa waandishi wa habari kutangaza azma yetu. Nilimshauri asubiri
kidogo kwani ilikuwa bado ni mapema mno kuweza kuviarifu vyombo vya
habari.
Taarifa hizi ziliendelea kubaki
kuwa siri hadi tarehe 26 Aprili, 1964 pale Redio ya Tanganyika
ilipotangaza kwamba siku hiyo Marais wawili hao watakutana katika Bunge
la Tanganyika kubadilishana Hati za Muungano ambazo zimeunganisha
Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja.
MISUKOSUKO KATIKA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Muungano wa Zanzibar na
Tanganyika umepita katika masaiba kadhaa tokea kuasisiwa kwake takriban
miaka 49 iliyopita lakini mtikisiko ulioukumba katika siku za karibuni
ni mkubwa sana. Ni mkubwa kwa sababu umegusa kiini cha Muungano huu
ambapo suala linaloulizwa ni iwapo kwa kule kukubali kushirikiana katika
baadhi ya mambo, je, Zanzibar na Tanganyika zimejifuta na hivyo
kupoteza hadhi zake kama nchi? Hilo limekuwa ndiyo suala kubwa
linaloulizwa na Wazanzibari hasa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda
kutamka Bungeni kwamba Zanzibar si nchi.
Muungano huu umekuwa gumzo kuu
katika takriban kila mjadala wa katiba na siasa katika nchi yetu.
Umejitokeza na kujionyesha hivyo katika mwaka wa mwanzo wa Muungano
kuhusiana na sakata la kuwa na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi
kwa upande wa Tanganyika na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa
upande wa Zanzibar, kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
mwaka 1964 – 1966.
Mengine ni wakati wa kuunganisha vyama vya ASP na TANU kuunda Chama
Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977, katika mjadala wa marekebisho ya Katiba
wa 1983/84 na hatimaye kujiuzulu kwa Rais wa pili wa Zanzibar Sheikh
Aboud Jumbe, wakati wa kuondolewa katika Uwaziri Kiongozi kwa mwandishi
wa maoni haya na hatimaye kufukuzwa katika CCM na wenzake 6 mwaka 1988,
katika harakati za madai ya kutaka kura ya maoni kuhusiana na Muungano
huo mwaka 1989/90, wakati wa mjadala wa kuanzishwa vyama vingi mwaka
1991.
Kama hayo hayatoshi misuko suko
mingine mikubwa ilijitokeza katika sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja
wa Nchi za Kiislamu (OIC) mwaka 1993, wakati wa mjadala wa G-55 kudai
kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994,
katika mjadala wa marekebisho ya 11 na 14 ya Katiba ya Muungano mwaka
1994/95, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 1995 na ule wa 2000 na
karibuni kabisa kuhusiana na suala la matarajio ya ugunduzi wa mafuta
visiwani Zanzibar, harakati za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki
na pia baada ya kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar
ya 1984 yaliyofanywa mwaka 2010.
Tume na Kamati kadhaa zimeundwa kuainisha matatizo ya Muungano na
kupendekeza njia za kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda
Tume na Kamati zifuatazo, miongoni mwa nyingi, kuhusiana na masuala
haya:
1. Kamati ya Mtei
2. Tume ya Jaji Francis Nyalali (1991)3. Kamati ya Shellukindo (1994)
4. Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
5. Kamati ya Jaji Mark Bomani (1995)
6. Kamati ya Jaji Robert Kisanga (1998)
7. Kamati ya ‘Harmonization’
8. Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo kwa upande wake iliunda Kamati zifuatazo kwa madhumuni hayo hayo:
1. Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992
2. Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna) ya 1997
3. Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman)
4. Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000
5. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje6. Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya 2001
7. Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
8. Kamati ya Mafuta9. Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania
10. Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ)
11. Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu
12. Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999)
13. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuyaondoa (2004)
Ukiacha Tume, Kamati na Ripoti
hizo, kuanzia mwaka 1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya Pamoja ya
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar pamoja
na Mawaziri wa Serikali zetu mbili ambao ulitarajiwa uwe ndiyo jukwaa
la kuzungumzia matatizo kutoka kwa washiriki wakuu wa Muungano huu na
kuyapatia ufumbuzi unaofaa.
Utaratibu huu uliachwa kwa muda
mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete
alilolitoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali
yake huko Ngurdoto, Arusha mwezi Februari, 2006. Mikutano hiyo sasa
imebadilishwa utaratibu wake na inaongozwa na kusimamiwa na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano na timu za pande mbili zikiongozwa na Waziri
Mkuu kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais kwa
upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
KIINI CHA MATATIZO YA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama tulivyokwisha kuona kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliundwa kupitia Mkataba wa Muungano wa 1964 (Articles of Union). Mkataba huu, kwa kutumia ushahidi wa picha, ulitiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, kwa niaba ya nchi zao mbili katika Ikulu ya Zanzibar, tarehe 22 Aprili, 1964.
Mkataba wa Muungano wa 1964 ni Mkataba wa Kimataifa na ndiyo maana kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kiingereza zilizokuwa zikifuatwa na Zanzibar na Tanganyika wakati huo na hadi leo uliweka sharti katika kifungu cha (viii) kwamba unapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar likishirikiana na Baraza lake la Mawaziri ili kuupa nguvu za kisheria ndani ya nchi mbili hizo.
Hoja ya kwanza inayojitokeza hapa
na ambayo imeshindwa kupatiwa majibu hadi leo ni kushindwa kupatikana
kwa nakala halisi ya Mkataba huo ikiwa na saini za Rais Nyerere wa
Jamhuri ya Tanganyika na Rais Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Hoja hii imeibuliwa ndani ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia katika Mahkama Kuu ya Zanzibar
ambako Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimeshindwa kutoa nakala hiyo licha ya kuahidi
kufanya hivyo.
Nusura pekee iliyobaki ni
kutegemea nakala halisi (iwapo ipo) inayoelezwa kwamba ilikabidhiwa kwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kumbukumbu za Umoja huo
kujiridhisha kwamba nchi mbili hizi zimeungana. Kuonekanwa kwa nakala
halisi ya Mkataba huo ni muhimu sana katika kujiridhisha uhalisia wa
kile kilichokubaliwa baina ya nchi zetu mbili.
Hoja ya pili ni ile inayohusu
utekelezwaji wa matakwa ya uthibitishaji (the want of ratification) wa
Mkataba huo kwa upande wa Zanzibar. Upo ushahidi wa kutosha kwamba Bunge
la Tanganyika lilikutana na kuuridhia Mkataba huo tarehe 25 Aprili,
1964. Kwa upande mwengine, hakuna ushahidi wowote kwamba Baraza la
Mapinduzi likishirikiana na Baraza la Mawaziri la Zanzibar lilikaa
kuuridhia Mkataba huo kwa kupitisha Sheria ya Kuthibitisha (Ratification
Decree) kama ilivyotakiwa na Mkataba wenyewe. Kwa hakika ushahidi
ulioibuliwa na Prof. Issa Shivji katika kitabu chake cha karibuni
kabisa, Pan-Africanism or Pragmatism? Lesssons of Tanganyika-Zanzibar Union umeweka wazi pasina chembe ya wasiwasi kwamba Mkataba huo haujaridhiwa na upande wa Zanzibar hadi hii leo.
Ukiachilia mbali hoja hizo, na
kwa msingi wa hoja tukichukulia kwamba Mkataba huo ni halali, bado
ukitazama kwa jicho la sheria, utaona kiini cha matatizo ya Muungano
kinatokana na tafsiri ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa
1964.
Mfumo uliopo sasa ambao ulianza
kutekelezwa 1964 ni ule wa serikali mbili – ile ya Jamhuri ya Muungano
na ile ya Zanzibar. Tanganyika haikuwekewa serikali yake tofauti;
madaraka yake kwa yale mambo yasiyo ya Muungano yalielezwa kwamba
yatasimamiwa na kuendeshwa na Serikali hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano.
Hata hivyo, uhalali wa kisheria wa muundo huu umeendelea kuhojiwa na
hata kupingwa kwamba hauwakilishi ipasavyo makusudio yaliyomo katika
Mkataba ulioanzisha Muungano wenyewe.
UVUNJWAJI WA MKATABA WA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Mbali na suala la muundo wa
Muungano, maeneo mengine mengi yanayogusa msingi wa Mkataba wa Muungano
yaliendelea kuvunjwa na Tanganyika ikivaa joho la Serikali ya Muungano.
Kifungu cha (iv) cha Mkataba wa
Muungano kiliorodhesha mambo 11 tu ambayo ndiyo yaliyokubaliwa na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kuwa mambo ya
Muungano. Hata hivyo, kipindi cha miaka 49 ya Muungano kimeshuhudia
mambo hayo yakiongezwa isivyo halali kwa kutumia chombo kisicho na
mamlaka ya kufanya hivyo yaani Bunge la Muungano na sasa kufikia 22
lakini ukiyanyumbua yanafikia 37.
Mfano unakuta kifungu kimoja cha
11 kinayaweka pamoja mambo manne ambayo ni Bandari, Usafiri wa Anga,
Posta na Simu. Kwa lugha ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman
Masoud Othman, anasema ni makontena 22 yenye mambo 37 ya Muungano.
Ikumbukwe kwamba kila hatua ya kuongeza mambo ya Muungano maana yake ni
kuchukua mamlaka ya Zanzibar na kuyahaulisha kwa Serikali ya Muungano
ambayo kama tulivyokwisha onyesha kwa hakika hasa ni Serikali ya
Tanganyika iliyojivika joho la Muungano.
Mambo hayo yaliyoongezwa juu ya
Makubaliano ya Muungano ya asili, yaani, yale kumi na moja (11) ni haya,
kama yanavyoelezwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano:-
1. Mambo yote yanayohusika na
Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti);
mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha
za kigeni.
2. Leseni za Viwanda na Takwimu.3. Elimu ya Juu.
4. Maliasili ya Mafuta, pamoja na
mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta aina ya petroli na aina
nyinginezo za mafuta au bidhaa za mafuta, na gesi asilia. 5. Baraza la
Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
6. Usafiri na Usafirishaji wa Anga.7. Utafiti.
8. Utabiri wa Hali ya Hewa.
9. Takwimu.10. Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
11. Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo.
Ukiondoa mambo hayo, yapo pia
mambo mengine ya ziada ambayo yameingizwa katika Muungano kwa Bunge tu
kutunga sheria na kutangaza kwamba zitatumika hadi Zanzibar.
Mfano wa masuala kama hayo ni
Uvuvi wa Bahari Kuu na Tume ya Utawala Bora na Haki za Bianadamu. Yapo
baadhi yake kwa mfano Usafiri wa Baharini ambapo Zanzibar ilikataa
kutekeleza sheria iliyopitishwa na Bunge na hatimaye ikatunga sheria
yake yenyewe kuhusiana na suala hilo.
Aidha, kuunganishwa kwa vyama vya
TANU na ASP na kuzaliwa CCM huku chama hicho kipya kikijipa madaraka
juu ya vyombo vyengine vyote vya maamuzi katika nchi ikiwemo Serikali na
Bunge na Baraza la Wawakilishi ilikuwa ni mtihani mkubwa na ukiukwaji
wa mkataba wa Muungano. Dhana hiyo ya Chama kushika hatamu iliyoasisiwa
na Mwalimu Nyerere, lengo lake lilikuwa ni kujilimbikizia madaraka yeye
na Chama alichokuwa akikiongoza kama milki yake binafsi.
Chini ya mfumo huo, CCM iliweza
kutoa maagizo na maamuru mazito bila ya kujali madaraka ya Serikali ya
Zanzibar yaliyotolewa kupitia Mkataba wa Muungano na hivyo kujinyakulia
uwezo wote wa kuitawala Zanzibar ipendavyo huku viongozi wa Zanzibar
wanaohoji wakituhumiwa kwamba wanapinga nidhamu ya Chama.
MATATIZO YATOKANAYO NA KIINI CHA TATIZOWaheshimiwa Waandishi wa Habari
Kiini cha tatizo la msingi la
Muungano ambalo kwa mtazamo wangu ni muundo wake unaotokana na tafsiri
potofu ya Mkataba wa Muungano ndicho kimepelekea kujitokeza kwa matatizo
mengine katika miaka 49 hii na ambayo yanaongezeka kila uchao.
Mtu anapoangalia matatizo au hizi
zinazoitwa kero, atagundua kuwa karibu yote yanatokana ama na mshirika
mmoja (mara nyingi Zanzibar) kutokuuamini au kuutilia shaka upande
mwengine, au mshirika wa pili (mara nyingi Tanganyika ikivaa joho la
Muungano), huku ikiamini kwamba ina haki ya moja kwa moja kuamua na
kutekeleza mambo fulani bila ya kulazimika kupata ridhaa ya upande wa
pili ambao inahisi kama imeubeba tu. Ukiangalia kwa undani utagundua
kuwa tatizo linarudi kwenye muundo.
Zanzibar haifahamu mamlaka ya Muungano katika Serikali ya Muungano
yanaishia wapi ambapo mamlaka kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa ajili ya
Tanganyika yanaanza.Tanganyika nayo kwa kuwemo kwake katika Serikali ya Muungano kunaifanya ishindwe kufahamu ni vipi na wapi Zanzibar inapata mamlaka ya kuhoji mambo ambayo yameshatamkwa kwamba ni ya Muungano hata kama hayakuwemo katika Mkataba wa asili wa Muungano. Hali hii inaonekana katika kila kile kinachoitwa “kero” za Muungano.
Mifano inaweza kutolewa kwa takriban mambo yote, lakini kwa madhumuni ya mkutano huu na waandishi wa habari tuchukue mifano ya mambo matatu yafuatayo yanayozusha malalamiko nayo ni:
1. Umilikaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
2. Uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano.
3. Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano.
NAFASI YA ZANZIBAR KATIKA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa HabariKwa kuendelea, ni vyema sasa tuangalie nafasi ya Zanzibar katika Muungano huu, hasa kufuatia kauli za kuidhalilisha Zanzibar zilizotolewa na wanasiasa wa Tanganyika hivi karibuni wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Kutokana na kule kule kujaribu
kujisahaulisha kuwepo kwa Mkataba wa Muungano ambao ndio sheria kuu
(grundnorm) ya Muungano na kuifanya Katiba inayoitwa ya Jamhuri ya
Muungano ionekane kuwa ndiyo Katiba mama na hivyo kuikweza kwamba eti
iko juu ya Katiba ya Zanzibar, zimetolewa kauli kwamba kufuatia hatua ya
kuungana na Tanganyika, Zanzibar imepoteza hadhi na sifa ya kuwa nchi.
Waliosema hivi wanasahau kwamba Zanzibar ina Katiba yake ambayo ina
hadhi sawa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, na kwamba zote mbili
zinapaswa kutafsiri kisawa sawa Makubaliano ya Muungano.
Katiba ya Zanzibar inatamka wazi
wazi kwamba Zanzibar ni nchi. Utangulizi wa Katiba hiyo ambao unaeleza
dhamira ya Wazanzibari wakiwa ndiyo wenye Katiba hiyo unabainisha wazi
wazi dhamira ya Wazanzibari kulinda na kudumisha nchi yao na yale yote
yanayoitambulisha Zanzibar kama nchi.
Huko nyuma kabla ya Marekebisho
ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyopitishwa mwaka 2010, ni
bahati mbaya kwamba baadhi ya watu walikuwa wakinukuu vibaya kifungu cha
(1) cha Katiba ya Zanzibar kilichokuwa kikisomeka kwamba, “Zanzibar ni
sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” kumaanisha kwamba kwa kuwa
kwake sehemu ya Jamhuri ya Muungano kunaiondolea na kuipotezea Zanzibar
hadhi yake ya kubakia kuwa nchi.
Tafsiri hiyo haikuwa sahihi kama ilivyofafanuliwa na Jaji Abdullahi
D. Zuru kutoka Nigeria, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kupitia
Sheria (Law Review Commission) Zanzibar.Jaji Zuru katika maelezo yake alisema kuwa anaamini kwamba waanzilishi wa hatua ya kuzileta pamoja Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja, hawajakusudia kuwa hatua hiyo ipoteze (erode) uhuru wa nchi yoyote kati ya nchi mbili kamili zilizohusika.
Kinyume na hayo, maoni yake ni kwamba nia ilikuwa kuimarisha uhuru wa kila moja ya nchi hizo mbili sambamba na ule wa Muungano utakaozaliwa. Mtaalamu huyo anafahamisha kwamba kisheria, “Haki mbili zikikutana ndani ya mtu mmoja, ni sawa na kusema kwamba ziko ndani ya watu wawili.”
Aidha, alisema ni imani ya Tume yake kabisa kuwa ulipoundwa Muungano, Zanzibar ilikusudia na ilisisitiza juu ya kuendeleza mamlaka yake ndani ya utaratibu wa Muungano. Na hapa namnukuu:
“Kutokana na haya, tunaamini kwamba hadhi ya Zanzibar kama inavyoelezwa katika kifungu cha (1) imepotoshwa kwa sababu (kifungu) hakielezi nia ya wenye katiba (sponsors of this constitution) na madaraka yaliyotolewa na watu wa Zanzibar…”
VIPI TUTOKE HAPA TULIPO?
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Inakaribia miaka 49 sasa tangu uundwe Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kulikuwa na wakati wa kutosha kurekebisha kasoro zilizopo. Hilo halikuwezekana kutokana na ubabe wa Mwalimu Nyerere ambaye aliamua kuwatia shemere Wazanzibari na kuhakikisha Muungano unakwenda kama alivyotaka yeye hata baada ya “kuondoka madarakani”.
Si jambo la kuficha kwamba wananchi wa pande zote mbili za Muungano wamechoshwa na unafiki uliopo na wanadai mfumo na muundo mpya wa Muungano utakaoweka misingi mipya ya ushirikiano.
Katika mijadala mbali mbali inayoendelea katika ukusanyaji wa maoni ya wananchi, vyama vya siasa na taasisi nyengine za kijamii kumetolewa hoja kwamba suluhisho la matatizo niliyoyafafanua hapo juu na mengine mengi yanayoukabili Muungano huu, kumejitokeza mapendekezo yanayoelekeza kwamba ufumbuzi wake ni muundo wa Serikali Moja, Serikali Mbili zilizopo sasa pamoja na marekebisho kadhaa au Serikali Tatu.
Kwa upande wa Zanzibar, wananchi
walio wengi wamependekeza kuwepo kwa Muungano wa Mkataba (Treaty based
Union) kama njia bora ya kudumisha mahusiano makongwe kati ya Zanzibar
na Tanganyika.
Kwa upande wangu, siamini kama Serikali Moja, Mbili au Tatu zitaweza
kumaliza matatizo yaliyopo ya Muungano na hasa kule kutokuaminiana
kukubwa kulikojengeka kutokana na matatizo hayo kuachwa muda mrefu bila
ya kushughulikiwa au kushughulikiwa kwa njia za hotuba za kisiasa zaidi
zisizofuatiwa na utekelezaji wowote. Sababu zangu za kutoiona mifumo
hiyo kama njia sahihi ya ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili ni hizi
zifuatazo.
Serikali Moja:
Mfumo wa Serikali moja umekuwa ukitajwa kuwa utaondoa manung’uniko na
kelele zote kuhusu matatizo ya Muungano lakini bado unaonekana kuwa na
matatizo yafuatayo:
1. Mfumo huu utazifuta kabisa
nchi za Tanganyika na Zanzibar na kuwa na nchi moja yenye mamlaka moja
inayosimamiwa na Serikali moja.
2. Ingawa mfumo huu unaweza kuungwa mkono na Watanganyika walio
wengi, Wazanzibari hawawezi kuukubali kabisa mfumo huu kwa sababu
utafuta utambulisho wao na historia yao.
3. Katika mfumo huu wa kuwa na
nchi moja yenye mamlaka moja, Zanzibar itachukuliwa kama eneo jengine
lolote la Tanzania na hivyo kutokuwa na uwezo wa kujiletea maendeleo
yake na badala yake itategemea maendeleo yatakayopangwa na Serikali kuu
kulingana na rasilimali zitakazotengwa kwa ajili ya eneo la Zanzibar
kama inavyopangwa kwa maeneo mengine.
Serikali Mbili:Mfumo wa serikali mbili uliopo hivi sasa una mkanganyiko wa mambo kadhaa kwa mfano:
1. Kutokuwepo kwa mshirika mmoja wa asili wa Muungano yaani Tanganyika. Hivyo linapotokea tatizo la Muungano badala ya kukutana pande mbili za Muungano na kujadiliana kwa misingi ya usawa sasa majadiliano yanakuwa baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Majadiliano ya namna hii yanakosa misingi ya haki na usawa.
2. Mabadiliko ya Katiba yaliyomuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano yalikwenda kinyume kabisa na makubaliano ya awali ya Muungano. Mabadiliko haya yanamuondoa mmoja wa washirika wakuu katika Serikali ya Muungano ambaye ni Rais wa Zanzibar.
3. Kumekuwa na mkanganyiko vile
vile kwa mambo ya Zanzibar ambayo siyo ya Muungano lakini mambo hayo
yanashughulikiwa na Serikali ya Muungano katika ngazi zote za kimataifa.
Kwa mfumo huu, Tanganyika inatumia jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kujifaidisha kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano katika
nyanja za kimataifa. Kama vile elimu, afya, kilimo, mazingira, michezo,
utamaduni, mawasiliano, miundombinu, usafiri baharini na angani.
4. Aidha, mfumo uliopo wa Serikali mbili hautoi fursa ya wazi kwa
upande mmoja wa Muungano (Tanganyika) kutetea maslahi yake ndani ya
Muungano.
5. Wabunge wa Zanzibar wanashiriki katika Bunge la Muungano kujadili mambo ambayo siyo ya Muungano.
6. Mfumo uliopo unaochanganya
mamlaka mbili (ile ya Serikali ya Muungano kwa mambo yote ya Muungano na
ile ya Tanganyika kwa mambo yake yasiyokuwa ya Muungano) unaleta
mkanganyiko mkubwa katika suala la kujua mipaka ya gharama za uendeshaji
wa Muungano na mapato yanayotokana na taasisi za Muungano.
Ushahidi mwengine wa wazi wa
kwamba mfumo uliopo umeshindwa kufanya kazi na wala hauwezi
kurekebishika ni kwamba katika miaka 20 iliopita kumeundwa Tume na
Kamati 8 kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Tume na Kamati
13 kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mbali na kuwepo kwa
Kamati ya Kudumu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwajumuisha
Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais (zamani
Waziri Kiongozi) wa SMZ lakini zote zimeshindwa kutatua matatizo ya
Muungano na badala yake yamekuwa yakizidi kila uchao.
Serikali Tatu:
Baadhi ya vyama vya siasa na hata
wasomi wa sheria wamekuwa wakipendekeza mfumo wa Serikali tatu
(Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar)
kama suluhisho la matatizo ya Muungano. Hata hivyo, mfumo huu nao kwa
sasa unaonekana bado hautaondoa manung’uniko kwa upande wa Zanzibar kwa
sababu:
1. Mfumo wa Shirikisho la
Serikali Tatu utatoa mamlaka ya ndani kwa nchi mbili zinazounda Muungano
huu na kuwa na Serikali zake za kusimamia mamlaka hayo lakini bado
mamlaka ya kidola yatabaki katika Serikali ya Muungano.
Madai makubwa yanayotolewa na
Zanzibar hivi sasa yanahusu kurejesha ‘sovereignty’ ili kuifanya
Zanzibar, serikali yake na viongozi wake wawe na hadhi ya kutambuliwa
kitaifa na kimataifa. Hilo halitapatikana katika mfumo wa Serikali tatu
kwa sababu:
2. Mamlaka yanayoshikiliwa na Serikali ya Muungano ambayo ndiyo
itakayoziwakilisha nchi mbili kimataifa bado ina nafasi kubwa ya kuweza
kutumika kumfaidisha mshirika mkubwa zaidi katika Muungano huo
(Tanganyika) kuliko kwa mshirika mdogo (Zanzibar) kwa kule tu kujiona
kwake ni mkubwa (big bro
No comments:
Post a Comment