Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif akitoa maoni yake juu ya katiba mpya
Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad leo amekutana na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kutoa maoni yake binafsi kuhusiana na mtazamo wake juu ya
katiba mpya ya Tanzania.
Maalim Seif ambaye amekuwa
kiongozi wa Kwanza mashuhuri kukutana na tume hiyo katika utaratibu wa
ukusanyaji wa maoni amesema katika kipindi cha miaka 49 ya Muungano bado
hakujakuwa na nia njema ya kutatua kero za Muungano, hali inayopelekea
kuongezeka kwa kero hizo na kuleta usumbufu kwa wananchi hasa wa
Zanzibar.
Amesema kutokana na hali hiyo ni
vyema muundo wa Muungano ukaangaliwa upya, na kusisitiza msimamo wake wa
kuwepo Muungano wa Mkataba ambapo kila nchi itakuwa na mamlaka yake
kamili ndani na nje ya nchi na baadae kushirikiana katika mambo ya
msingi ambayo yataamuliwa na pande hizo mbili.
Maalim Seif ambaye ametoa maoni
hayo nyumbani kwake Mbweni Zanzibar amefahamisha kuwa muundo wa Muungano
wa serikali mbili uliopo sasa hauwezi kutatua kero za Muungano baada ya
kuwepo kwake kwa kipindi cha miaka 49 bila ya kuonyesha mafanikio ya
kuridhisha ya kutatua kero hizo.
Amesema katika kipindi hicho tume
na kamati kadhaa zimeundwa katika kushughulikia kero za Muungano,
lakini mafanikio yake ni madogo, hali inayotia wasiwasi wa kuongezeka
kwa kero hizo badala ya kutatuliwa.
Amefahamisha kuwa Zanzibar
imekuwa muathirika mkubwa wa Muungano uliopo hasa katika Nyanja za
kiuchumi na siasa, baada mshirika wake wa Muungano (Tanganyika)
kutoweka, na kutumika jina la Tanzania kwa maslahi ya upande mmoja wa
Muungano.
“Koti la Muungano sasa linatubana
sana, na kwamba tunahitaji kushona koti jipya kulingana na hali zetu za
sasa”, alidokeza Maalim Seif
Maalim Seif anatarajiwa kukutana
na waandishi wa habari hapo kesho katika hoteli ya Bwawani Mjini
Zanzibar, ili kuyatolea ufafanuzi maoni hayo na kuyaweka bayana kwa
wananchi.
No comments:
Post a Comment