Serikali ya Somalia inatakiwa kumuachilia huru mara moja mwandishi wa
habari Abdulasis Abdinuur Ibrahim na watu wengine watatu wanaoshikiliwa
kuhusiana na mwanamke anayedai kubakwa na wanajeshi wa Somalia,
mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International, Kamati
ya Kuwalinda Waandishi wa Habari and Human Rights Watch yalisema katika
taarifa hapo Jumatano (tarehe 23 Januari).
"Serikali mpya ya Somalia inazungumza kwa usahihi kabisa kuhusu
utawala wa sheria na uhuru wa vyombo vya habari, lakini kuwafungia
waandishi wa habari na watu wengine wanaotoa taarifa kuhusu visa vya
ubakaji unatoa ujumbe tofauti na yale inayoyasema," alisema Mkurugenzi
wa Human Rights Watch barani Afrika Daniel Bekele. "Mamlaka ni lazima
iwaachilie huru watu hao wanne inaowashikilia na kuhakikisha kuwa polisi
wanachunguza ukatili wa kijinsia kwa ufanisi."
Mtu anayedaiwa kubakwa Lul Ali Hassan, Ibrahim pamoja na watu wengine
waliowezesha kukutana kwa Hassan na mwandishi Ibrahim wako mikononi mwa
polisi kwa muda wa wiki nzima sasa bila kufunguliwa mashtaka.
Katika kujibu tuhuma hizo serikali ya Somalia imerejelea ahadi yake ya kuwalinda waandishi wa habari na kuhakikisha kunakuwepo na uhuru wa kujieleza, huku ikitetea kitendo cha kumshikilia Ibrahim kwa ajili ya kuchunguza kisa hicho cha ubakaji dhidi ya Hassan.
Polisi ya Somalia imesema kuwa Ibrahim na makundi ya haki za wanawake
walimlipa Hassan ili atoe tuhuma za uongo dhidi ya vyombo vya usalama.
"Matokeo ya uchunguzi wa daktari yamethibitisha kuwa Lul hajabakwa
kama anavyosema mwenyewe na amethibitisha kwa hiyari yake kuwa tuhuma
hizo ni za uongo," alisema Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa,
Abdikarim Hussein Guled.
Umoja wa Waandishi wa Habari wa Somalia (NUSOJ) umeelezea wasiwasi
wake juu ya namna kesi hiyo inavyoendeshwa, hasa baada ya shauri
lililopangwa kusikilizwa Jumanne kuahirishwa kwa ombi la Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Abdulkadir Mohamed Ali Muse.
"Kwa niaba ya waandishi wa habari wa Somalia, natoa wito kwa serikali
ya Somalia kumwachilia huru mwandishi wa habari na kuunda tume huru ya
kuchunguza kwa umakini tuhuma hizo na kupata ukweli wa kesi hiyo,"
alisema Katibu Mkuu wa NUSOJ, Mohamed Ibrahim, kwa mujibu wa kituo cha
redio cha RBC cha Somalia.
No comments:
Post a Comment