Wednesday, January 23, 2013

Wakaazi wa Mtwara kutosikilizana na serikali ya Tanzania kuhusu mtambo wa gesi

Kwa mara ya tatu mwaka huu, wakaazi wa mkoa wa Mtwara nchini Tanzania wamekuwa na muungano wa umma kupinga mipango ya serikali ya kufunga bomba la mafuta kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda kwenye mitambo ya umeme ya Dar es Salaam.
  • Serikali ya Tanzania inapanga kuzalisha umeme kwenye mtambo huu katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam kwa kutumia gesi kutoka mkoa wa Mtwara. [Deodatus Balile/Sabahi]
Katika maandamano ya hivi karibuni ya tarehe 19 Januari, wakaazi walisema kazi zinazohusiana na rasilimali ya gesi iliyogundulika hivi karibuni lazima zibaki mkoani Mtwara na siyo kuzipeleka katika mji mkuu.
Salum Namkulala, mwenye umri wa miaka 62 mzaliwa wa Mtwara ambaye kwa sasa anafanya kazi Dar es Salaam, alisema serikali mara kwa mara imekuwa ikitelekeza mikoa ya kusini mwa Tanzania, ikiwaacha katika hali dhalili ya umaskini.
"Mtwara na Lindi ni mikoa yenye maendeleo kidogo katika nchi hii," Namkulala aliiambia Sabahi. "Kutoka uhuru wa [Tanzania], hatuna barabara, shule, hospitali au upatikanaji wa maji, na ajira ni balaa. Mtwara ni alama ya umaskini katika nchi yetu."
"Mwaka uliopita, Mungu aliamua kuubariki mkoa wetu uliotelekezwa kwa kutupa gesi," alisema. "Kwa mzaha, serikali imekuwa rafiki yetu, lakini inadumisha umaskini kwa kusafirisha gesi yetu kwenda Dar es Salaam. Kwa herufi kubwa tunasema 'hapana' kwa jambo hili."
Ili kuzalisha ajira na kugawa utajiri wa taifa kwa usawa, serikali inapaswa kujenga miundombinu ya kubadilisha gesi kuwa umeme mkoani Mtwara na kisha kuusafirisha kwenda sehemu nyingine za nchi hii, Namkulala alisema.
Mkaazi wa Mtwara Eligius Nakapanya, mwenye umri wa miaka 48, alisema ugunduzi wa gesi asilia katika mkoa huu ni fursa kwa maendeleo ya ndani kuliko kuunganisha rasilimali na fursa katika mji mkuu uliosongamana sana.
Kuendeleza sekta na kupata ajira huko Mtwara na mikoa mingine kutapunguza shinikizo la wahamiaji ambao wanakwenda Dar es Salaam kutafuta kazi, aliiambia Sabahi.
Mbunge Nimrod Mkono aliiambia Sabahi anaunga mkono kikamilifu msimamo wa wakaazi wa Mtwara kwa sababu sera za uchumi za Tanzania zimeshindwa kulinda maslahi ya ndani. Tangu serikali ilipofungua uchumi wake mwaka 1987 ili kuvutia wawekezaji, imezingatia katika kuandaa sheria za kuwalinda wawekezaji, alisema.
"Wawekezaji wana haki zaidi kuliko raia," aliiambia Sabahi. "Sera zetu lazima zimekosewa sehemu fulani, kwa namna fulani. Mtwara [wakaazi] wamejifunza kutokana na kilichotokea Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba katika mkoa wa Mara na hawataki kuingia katika mtego kama huo."
Katika mfano wake, kampuni binafsi ilichimba dhahabu kutoka Mara kati ya mwaka 1994 na 2004, lakini miaka michache baadaye mkoa uliendelea kuongoza katika maendeleo ndogo nchini ukiwa na shule chache, hakuna barabara za lami na hakuna hospitali.
Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini Hasnain Mohamed Murji alisema pia anaunga mkono msukumo wa wakazi wa kugawanya fursa kwa usawa.
"Viongozi wetu wanasema rasilimali zetu ni za chi nzima na hakuna mtu anayebisha hilo, bali tunachokisema ni kwamba nchi siyo Dar es Salaam tu," aliiambia Sabahi. "Vijana wetu wa kiume ni [wachuuzi] huko Dar es Salaam. Tunawataka warudi nyumbani Mtwara na kuwa mameneja wa viwanda."

Serikali yatetea msimamo wake

Rais Jakaya Kikwete amesema nchi nzima imefaidika na rasilimali zinazopatikana katika mikoa ya Tanzania.
"Mwanza na Shinganya imekuwa ikizalisha dhahabu, lakini haikuwahi kudai kufaidika peke yao na faida zote kutokana na dhahabu," alisema wiki iliyopita katika tukio la kufungua Uwanja wa Ndege wa Tabora uliyoboreshwa. "Mapato kutokana na dhahabu yanagawanywa kwa mikoa yote kupitia bajeti ya taifa."
Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo alisema suala la gesi limefanyika kisiasa na Watanzania wanapaswa kuepuka kuingiza siasa katika masuala ya msingi yenye faida kitaifa kwa sababu wanahatarisha kuiingiza nchi katika usumbufu.
"Wakati serikali ilipofanikiwa kupata mkopo wa dola bilioni 1 kutoka Benki ya Exim mwaka jana kwa ajili ya kujenga bomba, hakuna pingamizi lililotolewa," aliiambia Sabahi. "Ni namna gani tutafikia hatua ya utekelezaji, wanaanza vurugu hizi? Ninaweza kusikia dalili za siasa, na hili haliwezi kuwa zuri kwa taifa."
Muhongo alisema kupeleka gesi Dar es Salaam kunaleta maana kwa sababu jiji tayari lina miundombinu inayohitajika kubadilisha gesi hiyo kuwa umeme na kuingiza katika gridi ya umeme ya taifa. Kuruhusu mitambo yote ya umeme kufanya kazi katika uwezo kutasaidia kupunguza gharama ya umeme kwa nchi nzima, alisema.
Kwa kuwa viwanda vingi vya taifa vipo Dar es Salaam, alisema, kusafirisha gesi ghafi moja kwa moja kwenda mji mkuu kutapunguza gharama ya mitambo ambayo pia inatumia gesi kwa matumizi mengine.
Waziri alipuuza hoja za kupinga kwamba serikali inazingatia tu miradi inayolifaidisha mji mkuu na sio kushughulikia ukosefu wa ajira katika mikoa mingine.
Serikali inapanga kukamilisha utekelezaji wa mkakati wake wa maendeleo ya rasilimali ndani ya miaka kumi, alisema. Hii ni pamoja na kujenga maeneo ya viwanda katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambako gesi imegundulika. Mipango pia inajumuisha kujenga bandari huko Mtwara kwa ajili ya kuanzisha maeneo ya usafirishaji wa nje ya nchi na kujenga viwanda kwa ajili ya kutunzia gesi asilia iliyobadilishwa kuwa kimiminika na petrokemikali.
"Akili yangu inaniambia kwamba kama wanadai ajira, mipango niliyoitaja -- ambayo wanaitambua -- itazalisha ajira zaidi ya wanavyohitaji," Muhongo aliiambia Sabahi. "Wasiwasi wangu ni kwamba tunacheza siasa chafu."

No comments:

Post a Comment