Majengo ya michezo mjini Mogadishu kwa sasa yanafanyiwa ukarabati kufuatia miaka mingi ya kutotumiwa na kutotengenezwa.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Somalia (SFF), kwa ufadhili kutoka
Shirika la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), limeanza ukarabati wa
Uwanja wa Konis katika Wilaya ya Abdulaziz mjini Mogadishu.
Uwanja wa Konis ni moja miongoni mwa majengo makubwa ya michezo mjini
Mogadishu ambayo yaliharibiwa vibaya sana miaka 20 iliyopita. Katika
miaka iliyopita, uwanja huu ulikuwa alama ya matumaini na kurejea kwa
hali ya kawaida jijini kukifanyika shughuli kama vile mwaka mmoja tangu kuondoka kwa al-Shabaab kutoka kwa jiji hapo tarehe 6 Agosti na mafunzo ya timu ya kwanza ya Olimpiki ya Somalia kushiriki katika michezo baada ya miaka mingi.
FIFA ilituma mhandisi kutoka Netherlands kuongoza mradi wa ukarabati
katika uwanja wa Konis, kwa mujibu wa mwenyekiti wa SSF Abdiqani Said
Arab.
Nyasi bandia zilizotolewa na FIFA sasa zinawekwa katika uwanja, aliiambia Sabahi.
Gharama kamili za ukarabati wa Uwanja wa Konis bado hazijajulikana,
alisema, kwa sababu ujenzi unaendelea. Alisema kuwa SFF itatoa tangazo
za gharama hizo baada ya ukarabati kukamilika mwezi Januari.
"Tunapenda tuvifanyie ukarabati viwanja vyote vya michezo nchini,
lakini hatuwezi kutokana na ukosefu wa fedha," Arab alisema. "Hivi
karibuni tulikarabati kiwanja cha mpira wa kikapu wa Ex-Lujino katika
Wilaya ya Abdulaziz. Gharama za ukarabati zilikuwa zaidi ya dola 10,000,
ambazo zilitolewa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Hormuud ."
Arab alisema kuwa wanatafuta michango kutoka makampuni na mashirika
kusaidia kukusanya fedha na kukarabati majengo mengine ya michezo
jijini.
Haji Aweys Sheikh Adow, naibu mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
Wilaya ya Wadajir na mchezaji mpira aliyestaafu, alisema kuwa
amefurahishwa na kufufuka kwa michezo nchini Somalia na kukarabatiwa kwa viwanja vya Benadir, na kuongeza kuwa chama chake kinajishughulisha na juhudi kama hizo.
"Tunalipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu la Somalia kwa kuchukua
hatua za kurejesha utukufu wa zamani wa viwanja vyetu," Adow aliiambia
Sabahi.
Alisema kuwa miradi ya ukarabati ni hatua kubwa mbele, hatimaye
kuwezesha michezo ya Somalia kupata upya utukufu wake wa zamani na
kuiimarisha katika miaka ijayo.
Dadir Amin, mchezaji wa Timu ya taifa ya Somalia na timu ya Benadir
Telecom, alisema, "Nina furaha kupita kiasi kwa sababu sikufikiria daima
kwamba ningecheza katika kiwanja chenye nyasi bandia wakati nikiwa
nchini kwangu. Kama ujuavyo, uwanja wetu wa Konis sasa una nyasi
zinazofaa kwa ajili ya kuchezea na mipango sasa ni kuufungua haraka ili
tuweze kucheza kule katika msimu ujao wa ligi."
Amin alisema kuwa mpaka sasa wachezaji wa Somalia wanaoshindana nje
wamepoteza michezo kwa sababu walikuwa hawakuzowea kucheza katika
viwanja vyenye nyasi bandia. Mara tu Uwanja utakapokamilika kwa ajili ya
shughuli, alisema ana matumaini kuwa hilo litabadilika, na kuwapa
wanariadha wa ndani mazingira sawa na yale watakayokabiliana nayo katika
mashindano ya kimataifa
No comments:
Post a Comment