Friday, January 4, 2013

Serikali yamuanika Idd Simba kortini

simba


 
 
 
 
 
 
Rate This

UPANDE wa jamhuri katika kesi ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kulisababishia hasara Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) inayomkabili mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo, Idd Simba, na wenzake umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kuwa Simba alitumia sehemu ya fedha za mauzo ya hisa zilizouzwa kwa kampuni ya Simon Group  Limited kununulia gari lake binafsi.
Mbali ya Simba, washtakiwa wengine ni mkurugenzi wa bodi aliyewahi kuwa diwani wa Sinza na Katibu Mwenezi wa CCM, mkoa wa Dar es Salaam, Salim Mwaking’inda, na Meneja Mkuu wa Shirika hilo, Victor Milanzi, ambao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta,Mei 29, mwaka jana.
Akisoma maelezo ya awali mahakamani hapo, wakili wa serikali, Awamu Mbagwa, alidai kuwa  Agosti 31, 2009, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Simon Group Limited, Robert Kisena, aliwasilisha barua ya kusudio la kununua hisa 49 za serikali kwa  uongozi wa UDA.
Mbagwa alieleza kuwa  Septemba 2,  2009, mshtakiwa wa tatu (Milanzi) ambaye alikuwa Meneja Mkuu wa UDA, alisaini barua ikiielekeza Simon Group, kuwasilisha malipo ya awali ya sh milioni 400 kama ishara ya dhamira ya kununua hisa hizo.
“Pia barua hiyo ya Kisena  iliielekeza  kampuni ya Simon Group kuweka fedha  hizo katika akaunti binafsi ambayo ni 0210001002, inayomilikiwa na Simba katika benki ya Bank M, tawi la Sea View na barua hiyo ilieleza zaidi kuwa malipo hayo ya awali ya sh milioni 400, yangejumuishwa katika ununuzi wa hisa hizo,” alidai.
Alidai kuwa barua hiyo ilielekeza kuwa pesa hizo ziingizwe katika akaunti hiyo kwa maelezo kuwa akaunti za UDA zilikuwa na madeni mengi wakati mshtakiwa huyo akifahamu maelezo hayo ni ya uongo.
Wakili huyo alieleza kuwa kutokana na maelekezo hayo ya washtakiwa, Septemba 3, 2009, Kisena kwa niaba ya Simon Group aliingiza sh milioni 250  katika akaunti namba 0210001002 iliyoko Bank M, tawi la Sea View, inayomilikiwa na Idd Simba.
Alidai kuwa fedha  hizo zilihamishwa kutoka katika akaunti namba 2046600338 inayomilikiwa na Robasika Agro Products iliyoko katika Benki ya NMB, kampuni ambayo Simon Group Limited ni mwanahisa wake na kwamba baada ya   fedha hizo kuingizwa katika akaunti hiyo, siku hiyo hiyo Simba alitoa sh milioni 100  kwa kutumia hundi namba 125293.
Alidai kuwa siku iliyofuata, Septemba 4, 2009, Simba alihamisha fedha hizo kutoka katika akaunti yake namba 0210001002, kiasi kingine cha sh milioni 100 kwenda katika akaunti namba 0150000381 inayomilikiwa na kampuni ya Africarriers Ltd, katika Bank M.
“Kiasi hicho kilichohamishiwa Africarriers, kilikuwa sehemu ya malipo ya ununuzi wa gari aina ya Toyota Landcruser  VX, lenye namba za usajili T 561 BCX, ambalo hivi sasa limesajiliwa kwa jina la Simba,” alisisitiza Wakili Mbagwa.
Alidai kuwa awali kabla ya kuingizwa kwa kiasi hicho cha sh milioni 250, akaunti ya mshtakiwa ilikuwa na sh 3,329,242.88 tu.
Kwa mujibu wa Wakili Mbagwa, Novemba 26, 2009, Kisena aliingiza sh milioni 30 katika akaunti namba 6033500127 inayomilikiwa na Pride Tanzania, Makambako, NMB na baadaye sh milioni 20  kwa maelekezo ya Idd Simba.
Aliongeza kuwa  kiasi hicho cha fedha baadaye Desemba 4, 2009  na Januari 27, 2010, kilihamishiwa katika akaunti namba 4081300002, inayomilikiwa na Pride Tanzania, makao makuu ya NMB, mwisho wake zikaingizwa  katika akaunti binafsi ya Idd Simba namba 0210001002 na mchakato huu wote ulifanyika kwa maelekezo ya Idd Simba.
Januari 22, 2010, Kisena aliingiza tena sh milioni 20  katika akaunti namba 0210001002 ya Idd Simba, hivyo kufanya jumla ya fedha zilizoingizwa na Kisena kwa niaba ya kampuni ya Simon Group Limited, katika akaunti binafsi ya Idd Simba kama malipo ya utangulizi ya ununuzi wa hisa za UDA, kufikia sh milioni 320.
Hata hivyo  fedha hizi zote hazikufikishwa kwenye  akaunti za UDA badala yake ziliishia kutumiwa vibaya na washtakiwa hao watatu.
Alidai kuwa baada ya hayo yote kuwa yameshafanyika, Januari 28, 2010 katika mkutano wa bodi uliofanywa na Simba na wa pili, Mwaking’inda, kwa makusudi na wakijua, walipitisha uamuzi wa kuuza hisa 7,880,303 za UDA kwa Simon Group, ambazo hazikutolewa kwa mauzo na uamuzi huo wa bodi ulifikiwa bila kufuata utaratibu wa zabuni yenye ushindani.
Wakili Mbagwa alidai kuwa kutokana na uamuzi huo, Februari 11, 2010, mshtakiwa wa kwanza na wa tatu kwa kutumia vibaya nafasi zao, walisaini mkataba wa makubaliano ya mauzo na Simon Group  ya hisa 7,880,303 ambazo hazikuwa katika mchakato wa kuuzwa.
Alidai kuwa hisa hizo ziliuzwa kwa bei ya sh 1,142,643,935 tu kwa bei ya sh 145 kwa kila hisa ambayo alidai ilikuwa ni chini ya bei ya soko  kwa wakati huo ambapo bei ilikuwa sh 1513 kwa kila hisa na matokeo yake washtakiwa waliisababishia UDA hasara ya sh 8,422,076,940 (sh 8.4 bilioni).
Mshtakiwa wa kwanza, Simba, alikiri kumiliki akaunti hizo zilizotajwa katika benki hizo na kwamba Kisena aliingiza katika akaunti zake jumla ya sh milioni 320 kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo alikana kutumia sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kununulia gari na kwamba fedha hizo hazikuwa sehemu ya malipo ya uuzwaji wa hisa za UDA.
“Si  kweli mheshimiwa hakimu, ni uzushi na uongo kuwa hizo sh milioni 320  zilizoingizwa katika akaunti zangu zilikuwa malipo ya awali au ya aina yoyote katika ununuzi wa hisa za UDA,” alidai Idd Simba hata hivyo bila kufafanua kuwa zilikuwa ni za nini.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 4 na 5 mwaka huu itakapoanza rasmi kusikilizwa.
CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment