Msaidizi Kamishna wa Polisi wa Dar es Salaam Suleiman Kova alisema kuwa kuna maafisa wa polisi chini ya milioni moja nchini na kwamba walinzi binafsi wa usalama wanaziba pengo.
"Hatuwezi kufanyakazi tena kwa kujitenga. Idadi ya walinzi binafsi nchini inafikia milioni 1.2, ikilinganishwa na maafisa wa polisi walio chini ya milioni moja," aliiambia Sabahi. "Walinzi binafsi wamekuwa muhimu sana katika kudumisha usalama na sasa tumeamua kuwapatia mafunzo kama ya polisi."
Polisi wanashirikiana na walinzi wa usalama kutoa huduma za ulinzi katika majengo muhimu ya serikali na asasi za hadhi ya juu kama Benki ya Tanzania, ofisi za ubadilishaji pesa, ofisi za wizara na makampuni kadhaa, Kova alisema, na kuongeza kuwa si busara kuwadharau maafisa wa ulinzi binafsi na kutowapa msaada ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na viwango sawa na polisi wa taifa.
Walinzi binafsi watahudhuria kambi ya mafunzo ya miezi sita inayosimamiwa na polisi. Mafunzo yatagharimu shilingi 600,000 (Dola 380) kwa mlinzi, kwa gharama kugawanywa kati ya mashirika binafsi na polisi, Kova alisema.
Alisema kuwa kampuni 10 zimeahidi kushiriki katika mpango huo na polisi wanatarajia walinzi wa usalama 50,000 watashiriki katika sehemu ya kwanza ya mafunzo yaliyopangwa kuanza tarehe 15 Febuari.
Waziri wa Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi alisema kuwa kupitia ushirikiano wa umma na bianfsi, Tanzania inavutiwa na walinzi binafsi kama washirika muhimu katika kudumisha usalama.
"Walinzi binafsi sasa wanapangiwa karibu katika kila pahali," Nchimbi aliiambia Sabahi. "Popote panapotokea tukio [la wizi] wao hujibu mara moja, na kwa msaada wa polisi majambazi wanajua kuwa hawana popote pa kujificha kwa vile nchi iko salama zaidi."
Mipango ya ushirikiano ilianza mwaka jana kwa kuanzishwa maafisa wa polisi jamii, ambao wamefanikiwa sana, alisema. Katika mpango huo, maafisa jamii wanafanyakazi kama polisi wa cheo cha kutoa msaada wakiwa na jukumu la kudumisha sheria na taratibu katika maeneo ya makazi ya watu.
Nchimbi alisema mafanikio yaliyofikiwa chini ya mpango huu yaliitia moyo serikali kupanua mpango na kuwapatia mafunzo walinzi binafsi ili kufikia viwango vya mafunzo ya polisi.
Walinzi binafsi ni muhimu kwa usalama wa taifa
Shahani Mokili, mlinzi mkuu wa Kampuni ya Speed Security, aliiambia Sabahi kuwa alifurahishwa kwamba serikali imetambua umuhimu wa walinzi binafsi wa usalama.Alisema kuwa walinzi binafsi ni muhimu kwa usalama wa taifa kwa sababu kwa kawaida wanapangiwa maeneo ya hatari kubwa na wanapaswa kupatiwa mafunzo kama ya maafisa wa polisi ili kugundua shughuli za uhalifu.
"Wezi wanalenga mabenki, ofisi za kubadilisha pesa na kampuni zenye fedha. Ikiwa utapita katika jiji hili maeneo yote haya yanalindwa na walinzi [binafsi]," Mokili aliiambia Sabahi. "Tunahitaji ustadi maalumu wa kupambana na uhalifu. Ninalipenda wazo la kutupatia mafunzo ili kuwa na ujuzi sawa na maafisa wa polisi."
Thadeus Ngorika, mwenye umri wa miaka 46, mlinzi katika kampuni ya Group Four Security anayefanyakazi katika City Bank huko Dar es Salaam, alisema pendekezo la mafunzo litajazia juhudi za ushirikiano baina ya polisi na walinzi binafsi.
Kwa kawaida wananchi wanajisikia raha kuzungumza na walinzi binafsi kuliko na polisi, aliiambia Sabahi, jambo ambalo linaweza kuwa la msaada wakati wa uchunguzi.
"Kimaumbile watu wanawaogopa polisi," alisema. Watu wanawachukulia walinzi binafsi kama raia, kwa hivyo watawasogelea wakiwa na taarifa za usalama lakini walinzi baadaye wanazipeleka kwa polisi, alisema.
No comments:
Post a Comment