Imewekwa na Mhammed Khamis
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiweka mchanga
katika kaburi kwa ajili ya kumzika marehemu Hashul Nassor katika
makaburi ya Nyamanzi, Wilaya ya Magharibi Unguja.
Maelfu ya wananchi wakiongozwa na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,
wamejumuika katika mazishi ya Mbunge wa Zamani wa jimbo la Ziwani (CUF),
marehemu Hashul Nassor.
Marehemu Hashul ambaye pia ni
mwalimu wa siku nyingi katika visiwa vya Zanzibar, amefariki dunia
katika hospitali ya Mnazimmoja na kuzikwa katika makaburi ya Nyamanzi
Wilaya ya Magharibi Unguja.
Akizungumza katika mazishi hayo,
Mkurugenzi wa Habari na Haki za Binadamu wa CUF Bw. Salim Bimani amesema
marehemu Hashul ametoa mchango mkubwa katika chama hicho na taifa kwa
jumla.
Amefahamisha kuwa marehemu Hashul ni miongoni mwa waanzilishi wa CUF na siasa za vyama vingi Tanzania, na aliwahi kuwa Mbunge wa Ziwani kupitia CUF katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 hadi 2000.
Wananchi
mbali mbali wakimsalia marehemu Hashul Nassor katika msikiti wa Kibweni
“Silver sand”. Marehemu alifariki jana katika hospitali kuu ya
Mnazimmoja na kuzikwa katika makaburi ya Nyamanzi, Wilaya ya Magharibi
Unguja. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Hadi kufariki kwake marehemu alikuwa mtendaji wa CUF na afisa mafunzo ndani ya chama hicho.
Pia amewahi kuwa mwalimu wa siku
nyingi wa masomo ya sayansi na alifundisha skuli mbali mbali za Unguja
na Pemba ikiwemo Skuli ya Sekondari ya Fidel-Castro.
Bimani alisema CUF kimempoteza
mtu muhimu ndani ya chama hicho ambaye alikuwa akitoa mchango mkubwa
hasa katika masuala ya taaluma.
Marehemu Hashul alifariki dunia
jana alfajiri (04/02/2013) katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja baada ya
kusumbuliwa na matatizo ya moyo.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi (Ammin).
No comments:
Post a Comment