Sunday, February 10, 2013

Walinzi wa pwani wa Somaliland wakamata meli za uvuvi za Kiyemeni

Walinzi wa pwani wa Somaliland siku ya Ijumaa (tarehe 8 Februari) walikamata boti zilizokuwa zikiendeshwa na raia wa Yemen waliokuwa wanafanya uvuvi kinyume cha sheria nje ya bahari ya Somaliland.
Katika operesheni hiyo iliyofanyika katika wilaya ya Karin, kilomita 100 mashariki ya Berbera, walinzi wa pwani waliwakamata wavuvi 32, kwa mujibu wa mkuu wa ulinzi wa pwani Somaliland Admirali Ahmed Osman Abdi.
"Walikuwa wanajishughulisha na uvuvi haramu katika bahari ya Somaliland na tutawashtaki kwa mujibu wa sheria," Abdi aliiambia Sabahi, na kuongeza kuwa wameshapelekwa Berbera kukabiliana na mashtaka.
Ingawa Waziri wa Uvuvi wa Somalialand ameziruhusu baadhi ya boti za uvuvi, wavuvi wa Yemen wamekuwa wakikiuka sheria kila mara, Abdi alisema. "Katika siku za karibuni, pia tuliwakamata wavuvi kadhaa wa Yemen wakivua haramu, na wamehukumiwa mahakamani," alisema.
Somaliland haipingi kuwepo kwa boti za uvuvi za kigeni, lakini zinalazimika kupata vibali halali, Abdi alisema.

No comments:

Post a Comment