Wednesday, February 6, 2013

Watu wenye silaha wampiga risasi afisa wa polisi Garissa

Watu wenye silaha walimpiga risasi na kumuua afisa mmoja wa polisi wa Kenya mjini Garissa usiku wa Jumatatu (tarehe 4 Februari), maafisa wa polisi waliiambia Sabahi.
Wauaji hao wanashukiwa kuwa na mafungamano na al-Shabaab, na wanaweza kuwa sehemu ya genge linalowalenga maafisa wa usalama wa Kenya kwenye eneo hilo, alisema mkuu wa wilaya ya Garissa Mohamed Maalim.
Maalim alimtaja afisa huyo kuwa ni Sajenti Mohammed Bolu Wako wa kitengo cha upelelezi cha Polisi wa Utawala katika kambi za wakimbizi za Dadaab.
"Alikuwa ndio kwanza amewasili kutoka Nairobi kuripoti kwenye kituo chake cha kazi siku ya Jumatano," Maalim aliiambia Sabahi. "Alikuwa anafanya kazi zake nje ya hoteli karibu na kituo cha mabasi alipopigwa risasi."
Maalim alisema polisi wamekuwa wakiwahoji mashahidi ili kujua lengo la mauaji hayo. Aliwatolea wito wakaazi wa huko kuwasaidia polisi kuwatambua na kuwakamata wauaji.
Al-Shabaab imewakodi wenyeji wa huko kuwalenga wanajeshi na polisi wa Kenya, alisema Maalim kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya. "Haiwezekani kwa al-Shabaab kutoka Kismayu na kuja kuanza kuua watu hapa," alisema. "Wahalifu hawa wanakodiwa na kundi hilo la kigaidi kusababisha mvutano katika mji huo."

No comments:

Post a Comment